BABA LEVO NI HABARI NYINGINE KIGOMA, ATUMIA DAKIKA 10 KIBABE MBELE YA DK.SAMIA

*Azungumza yaliyofanywa na Rais Dk Samia Kogoma ,aitaja mifupa migumu 

*Asema kwa Kigoma Mjini saa tano asubuhi tu anakabidhi jimbo kwa Dk.Samia

*Aomba barabara za lami katika mitaa ya Kogoma,masoko ya usiku

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Kigoma

DAKIKA 10 ambazo zimetumiwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Clayton Chipando maarufu Baba Levo kuelezea matamanio yake ya maendeleo ya jimbo hilo ambapo ameeleza kwamba Wana Kigoma wanaimaini kubwa na mgombea urais kupitia CCM Rais Dk.Samia Suluhu Hassani.

Kwa mujibu wa Baba Levo ambaye anagombea ubunge kupitia CCM amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi Rais Dk.Samia Suluhu Hasssan amefanikiwa kutafuna mifupa migumu ambayo imewasumbua kwa muda mrefu wananchi wa Kigoma.

Katika dakika 10 za Baba Levo mbele ya Mgombea urais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema chini ya uongozi wa Rais Samia Serikali yake imefanikiwa kutatua changamoto ambazo kwa muda mrefu zilionekana kuwa mfupa mgumu katika Mkoa wa Kigoma.

Baba Levo aliuteka mkutano huo kwa kueleza mazuri ambayo yamefanywa na Rais Samia ambapo alitumia dakika 10 hizo kuelezea hatua kwa hatua maendeleo yaliyofanywa na Serikali  huku maelfu ya wananchi wakiwa makini kufuatilia.Alianza kuzungumza saa 12:20 mchana hadi saa 12:30 mchana.

“Kazi ulizozifanya tulikuwa tunaziita mfupa mgumu, lakini kwako zimekuwa biskuti. Mashahidi wa haya ni wananchi wa Kigoma.Upatikanaji wa maji safi na salama umeboreshwa kwa kiasi kikubwa tangu Rais Samia aingie madarakani. 

“Dada zetu walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita mbili kutafuta maji, hali iliyowachosha kimwili na kuwafanya wazeeke kabla ya wakati,”amesema Baba Levo tena akijiamini na lile Vibe la Kigoma ndio kabisa

Kuhusu nishati, Baba Levo amesema kuwa tatizo la umeme katika mji wa Kigoma limepatiwa ufumbuzi baada ya kuunganishwa na gridi ya Taifa. “Tangu nimezaliwa tumekuwa tukihangaika na majenereta. Leo hii Mama umelizima na umetufungamanisha na umeme wa Taifa,” alisema.

Kuhusu maboresho yanayoendelea katika Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Baba Levo amesema Serikali imeonyesha dhamira ya kweli kwa kuleta wataalamu na vifaa vya ujenzi kuhakikisha eneo hilo linaboreshwa kwa viwango vya kisasa.

Pamoja na kupongeza mafanikio yaliyopatikana, Baba Levo ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangazia changamoto zilizobakia, hasa katika sekta ya barabara, masoko na fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo

 “Mfupa mwingine ni barabara. Vumbi ni tatizo kubwa. Tunaomba barabara ya kilomita 75 ili kurejesha hadhi ya Kigoma Mjini. Tuna imani kuwa huu nao utakuwa biskuti,” amesema.

Baba Leo ambaye pia anafahamika kwa jina la Baba la Baba na sasa Kibarabara ameomba pia kujengwa kwa soko la kisasa katika Kata ya Kibirizi na kuboreshwa kwa masoko ya jioni ili kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kufanya biashara katika mazingira salama na ya heshima.

Baba Levo alimshambulia mpinzani wake Zitto Kabwe kwa maneno ya kejeli, akisisitiza kuwa ushindi wake uko wazi.“Mtu ninaeshindana naye ni dhaifu sana. Tutampiga saa tano na nusu, tukabidhi asubuhi”

 Kuhusu kilio cha fidia kwa zaidi ya Sh.bilioni 8 kwa wananchi waliopisha ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Kigoma ameomba Rais Samia kusaidia katika kufanikisha malipo hayo na kwamba matanio yake ni kuona wananchi wanalipwa fidia na ndege zinapotua wawe wanafurahia badala ya kununa.

Pamoja na hayo Baba Levo amemuomba Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuyafanyia kazi maombi yake katika jimbo .”Yamekuwa yakisema mengi kuhusu mimi nakuomba Mwenyekiti na mgombea wetu wa urais maombi yetu wana Kigoma,nataka niwaoneshe Baba Levo anavyopigania maendeleo ya wananchi wa Kigoma Mjini.”