Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameipongeza CRDB Bank Foundation kwa kufanikisha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mfumo jumuishi, inayowanufaisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam, ambapo hadi sasa jumla ya Sh bilioni 2.9 imetolewa.
Mpogolo ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki, wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki 11 zenye thamani ya Sh44 milioni kwa vikundi viwili vya Titanic Bodaboda The Posh na Bodaboda Kisgo. Pikipiki hizo zimekatiwa bima kubwa na kufungwa vifaa vya ufuatiliaji.
“Wakati ninyi mnapokea pikipiki leo, wapo wengine wanatengeneza samani baada ya kupata mkopo wa Sh150,000 na kikundi kingine cha vijana watano kilichopewa Sh700,000 sasa thamani yake imefikia zaidi ya Sh850 milioni. Haya yote ni matokeo ya dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaunganisha vijana kiuchumi,” amesema Mpogolo.
Aidha, amewataka wanufaika kuzingatia utaratibu wa kuomba mikopo hiyo na kuimarisha nidhamu ya matumizi.
Amesisitiza umuhimu wa kuwa na leseni, bima kubwa na mifumo ya ufuatiliaji ya kidijitali kwa vyombo vya moto, ili kuhakikisha ulinzi na uthabiti wa uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuziamini taasisi za fedha kusimamia mikopo hiyo na Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, kwa kuipa CRDB Bank Foundation nafasi hiyo.
Mwambapa amesema tangu mwanzo wa mwaka huu wamepokea maombi kutoka zaidi ya vikundi 120 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam, ambavyo vimepewa pia mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha kabla ya kukopeshwa.
“Ushirikiano huu umewawezesha wajasiriamali wengi kunufaika na mikopo jumuishi, na CRDB Bank Foundation imeunganisha mifumo yake na ule wa Serikali wa Wezesha ili kuongeza ufanisi,” amesema.