MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema fidia kwa wananchi kwa waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege mkoani Kigoma watalipwa kwani Serikali ya Chama hicho haitamdhulumu mtu.
Dk.Samia ametoa kauli hiyo leo Septemba 14,2025 alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi wa Jimbo la Kigoma Mjini mkoani Kigoma ambapo mgombea ubunge wa jimbo Clayton Chipando maarufu Baba Levo ambaye alitoa ombi kwa Rais Samia kuhusu malipo ya fidia kwa wananchi hao.
Amesema kuwa wanaodai fidia watalipwa na kama kuna maeneo ambayo ya wananchi yamechukuliwa serikali italipa fidia.
“Tunafanya uchambuzi na uhakiki. Kwa zile ambazo tunahakika ndizo thamani yake, tutakuja kuzilipa. Serikali ya Chama Cha Mapinduzia haidhurumu mtu, tutakuja kuzilipa Fidia zote,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk.Samia amezungumzia kuhusu wafugaji ambapo amesema kazi kubwa imefanya kazi na ahadi ya serikali kwa jamii hiyo ni kuendeleza ujenzi wa majosho, mabwawa kwa ajili ya mifugo, chanjo na kuboresha machinjio.
Kwa upande wa uvuvi, amesema Serikali imeanza kuleta vizimba na boti ambavyo kwa sasa katika mkoa huo, vizimba 26 tayari vipo Pamoja na boti mbili za uvuvi.
“Mtakapotupa ridhaa, tutaongeza mikopo kwa ajili ya boti na vizimba ili tuzidi kuvua Samaki wengi kupeleka sokoni. Tutaendelea kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo.
“ Pamoja na mikopo itakayotolewa na halmashauri, wakati nikizindua kampeni nilisema tutatenga sh. bilioni 200 kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara ndogondogo.
“Tumejipanga kutimiza ahadi yetu ya muda mrefu ya kuboresha vibanda vya machinga Kibirizi, kazi hiyo tumewapa Wizara ya Uchukuzi wanapoendeleza na kuboresha bandari ya Kigoma wafanye na hilo.
“Mamlaka ya bandari ndiyo yenye jukumu la kuboresha vibanda hivyo na sisi tutakwenda kuwakumbusha ili waanze na hilo wakati wanaendelea na mambo mengine,” amesema.
Kuhusu changamoto ya mafuriko, amesema mkoa huo nyakati za masika umekuwa ukikumbwa na mafuriko hususani Kaya ya Katibuka ambapo chanzo cha tatizo hilo ni kuongezeka maji katika bwawa la Katibuka linalopokea maji katika maeneo mbalimbali ya mji wa Kigoma.
Amewaambia wananchi hao tayari serikali imeanza kushughulikia kero hiyo ambapo inakwenda kuondoa kabisa changamoto hiyo.
Kwa upande wa Vilevile, changamoto ya vivuko vya wananchi wa kata tatu zilizopo wilayani Kigoma ambazo zinafikika kwa njia ya maji pekee kupitia Ziwa Tanganyika, ambapo ameahidi kulitafutia ufumbuzi kwa kuleta kivuko bora kinachokidhi mahitaji ya wananchi.