Mbeya. Mgombea ubunge wa Jimbo jipya la Uyole kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Tulia Ackson, ametaja vipaumbele 15 ambavyo amesema vitabadili taswira ya Uyole ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa halmashauri mpya itakayojitegemea kimapato.
Ametoa kauli hiyo jana Jumamosi, Septemba 13, 2025, katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika Shule ya Msingi Hasanga, alipokuwa akiomba kura na kueleza utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025/2030.
Miongoni mwa vipaumbele alivyoainisha ni ufungaji wa kamera za usalama, upanuzi wa barabara kutoka Uyole hadi Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi, ujenzi wa vituo vya afya, upatikanaji wa vifaa tiba, nyumba za watumishi wa afya na maboresho ya reli ya Tazara.
Dk Tulia, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, amesema vipaumbele hivyo vinahusisha pia ununuzi wa magari ya wagonjwa kwa Hospitali ya Wilaya ya Igawilo pamoja na vituo vya afya vilivyopo na vitakavyoanzishwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo endapo CCM itapata ridhaa.
Amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi kutokana na ongezeko kubwa la watu katika Bonde la Uyole, hususan huduma za afya kwa akinamama wajawazito.
“Tutandelea na utaratibu wa kutoa bima za afya kwa wananchi wasiojiweza na kusukuma mbele ajenda ya kujenga vituo vya afya katika maeneo ya Ilomba, Nsalaga na Uyole, vikijumuisha dawati la malalamiko kwa wajawazito,” amesema.
Dk Tulia amebainisha kuwa Serikali inakusudia kukamilisha mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira wenye thamani ya zaidi ya Sh119 bilioni, pamoja na mradi wa Ilunga utakaosambaza huduma ya maji Jiji la Mbeya na Uyole.
Aidha, ameeleza kuwa visima vipya vya maji vitachimbwa maeneo ya Nsalaga, Itezi, Ilindi, Gombe Kaskazini, Shule ya Sekondari Iduda, Ilemi na Kituo cha Afya Iyela, ili kupunguza kero ya upatikanaji wa maji safi.
Kuhusu nishati, amesema Serikali imepanga ndani ya miaka mitano ijayo kuhakikisha huduma ya umeme inafika katika mitaa yote ya Uyole, ikiwemo Mwasanga ambapo tayari transfoma imefungwa na kinachosubiriwa ni kuwasha umeme.
Dk Tulia pia ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kujenga kituo cha maonyesho ya Nanenane na soko la kimataifa la mazao katika Kata ya Isyesye kwa lengo la kufungua fursa kwa wakulima.
Amesema endapo CCM itashinda, ajenda ya kilimo itasogezwa mbele kwa kuhakikisha Chuo cha Kilimo Uyole kinatoa elimu kwa wakulima na kuvutia wawekezaji kujenga maghala makubwa ya kuhifadhia mazao.
“Lengo ni kusaidia wakulima kutunza mazao kama ndizi na viazi yasiharibike wakisubiri masoko. Pia tutaboresha miundombinu ya barabara na kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu,” amesema mgombea ubunge huyo.
Kwa upande wa elimu, amesema Serikali imeahidi kujenga matundu ya vyoo 704 katika shule za msingi, kukarabati ofisi za walimu, pamoja na kujenga na kukarabati vyumba vya madarasa 1,600, kati ya hivyo 1,100 vitakuwa vya shule za msingi.
Aidha, amesema nyumba 55 za walimu zitajengwa katika shule za msingi na sekondari, pamoja na kutengeneza madawati 550,000, ambapo 300,000 kati ya hayo yatapelekwa shule za msingi.
“Wananchi wa Uyole, nikisema ‘kazi’ mnaitika ‘kazi’, lakini yote haya ni matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita. Ombi langu kwenu ifikapo Oktoba 29, 2025, ni mnipatie kura zenu za kishindo mimi na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini, Humphrey Msomba, amesema Dk Tulia ni mgombea wa mfano kwa namna alivyojitoa kuleta maendeleo, licha ya kuwa tayari kutekeleza sehemu kubwa ya Ilani ya Uchaguzi.
“Mwaka 2020 tulipomchagua kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini tulikuwa nyuma kimaendeleo, lakini leo tunashuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanyika kwa vitendo,” amesema Msomba.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo, amewaomba wananchi kumpa kura Dk Tulia pamoja na mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan ifikapo Oktoba 29, 2025, siku ya uchaguzi mkuu.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wamempongeza mgombea huyo, akiwamo mfanyabiashara wa matunda Kituo cha Mabasi Tukuyu, Subira Mwakyusa ambaye amesema: “Dk Tulia hana haja ya kuomba kura, kwa sababu kazi alizozifanya tayari ni ushindi unaojitosheleza.”