KOCHA wa Yanga, Romain Folz kwa mara ya kwanza kesho anatarajiwa kuiongoza timu hiyo kuvaana na Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii, huku mwenyewe akisema kikosi alichonacho kipo tayari kwa mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu mpya wa 2025-2026 licha ya ugeni wake nchini.
Yanga na Simba zitavaana kesho katika Dabi ya Kariakoo ya Ngao ya Jamii ikiwa ni siku 83 tangu zilipoumana mara ya mwisho Juni 15 likiwa ni pambano lililofungia msimu wa Ligi Kuu 2024-2025 na Mnyama kunyooshwa mabao 2-0 ya Pacome Zouzoua na Clement Mzize.
Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kuichapa Bandari Kenya bao 1-0, Folz alisema ameridhishwa na maandalizi kwa jumla ya timu hiyo kwa ajili ya mechi ya kesho akiwataka mashabiki waendelee kuwaunga mkono kwa kujitoa kwa wingi Kwa Mkapa.
“Tumecheza kwa kujituma na nimejaribu kuwapa muda wachezaji wote ili mashabiki waweze kuwaona,” alisema na kuongeza;
“Kuna mengi ya kufanyia kazi, lakini kwa jumla si vibaya. Tuna nafasi ya kuboresha zaidi kabla ya mechi kubwa iliyoko mbele yetu.”
Kuhusu maandalizi ya dabi dhidi ya Simba, kocha huyo alisema: “Ni mechi kubwa. Ikiwa tutaingia kwa undani zaidi wa maandalizi tunaweza kuzungumza hadi kesho. Lakini niseme tu tunajipanga vizuri na tunaamini tuna nafasi nzuri ya kushinda. Tupo tayari kwa vita hii.”
Kocha huyo aliongeza mechi dhidi ya Simba itakuwa kipimo kizuri kwa kikosi hicho ambacho kimekuwa kikiimarishwa katika kipindi cha maandalizi ya msimu.
Alisema ni mechi ambayo itatoa burudani kwa mashabiki kutokana na ubora wa timu zote mbili.
“Simba ni wapinzani wazuri, lakini na sisi pia ni timu bora. Sijawahi kukutana nayo, wala kuifuatilia sana, lakini nimeiona ikicheza katika mechi zao,” alisema na kuongeza;
“Tutafanya kila kitu kuhakikisha tunapata ushindi. Ni mchezo wa kuvutia na nina uhakika mashabiki watafurahia.”
Folz pia aliwapongeza mashabiki wa Yanga kwa sapoti kubwa waliyoonyesha katika mechi ya kirafiki na anaamini watajitokeza tena kwa wingi kwenye dabi.
“Tuna furaha kubwa kuwa na mashabiki wetu,” alisema. “Tunajivunia kuwaona wakituunga mkono kila mara, na tunawakaribisha kwa wingi zaidi katika mchezo dhidi ya Simba. Ni nyinyi mnaotupa nguvu ya kupambana.”
Mechi ya kesho Jumanne itakuwa ya kwanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na tayari mashabiki na wadau mbalimbali wa soka nchini wanaiangalia kama kipimo cha nani atakuwa na mwanzo mzuri kati ya miamba hiyo miwili ya Tanzania.
Yanga, itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya mafanikio ya misimu minne iliyopita, huku Simba nao wakitazamia kuanza msimu kwa kishindo wakitaka kurejesha heshima yao.
Kwa mujibu wa Folz, kikosi chake kimepata nafasi nzuri ya kuimarisha mshikamano kupitia mechi za kirafiki, jambo analoamini litakuwa silaha muhimu kwenye mechi hiyo.
Katika mechi tano zilizopita katika mashindano yote, Yanga inarekodi ya ushindi wa asilimia 100 dhidi ya Simba, ikishinda zote huku ikiwa na wastani wa kufunga mabao mawili.