Unguja. Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi ya chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa, amesema hoja tatu ikiwemo uzalendo na uaminifu ndizo zinazombeba mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, Othman Masoud Othman.
Hoja nyingine ni uwajibikaji na kiongozi anayejali maisha ya Wazanzibari, akitaka waishi vizuri.
Ameeleza hayo leo Jumapili, Septemba 14, 2025, wakati wa ufunguzi wa kampeni za urais wa Zanzibar za Othman kwa upande wa Unguja, uwanja wa Kibanda Maiti, baada ya jana Jumamosi kuzindua kampeni kisiwani Pemba katika uwanja wa Tibirinzi, wilayani Chakechake.
“Uchaguzi huu utaamuliwa na hoja tatu zitakazowaongoza wapigakura wa Zanzibar wakifika kwenye sanduku la kura. Nataka mkifika kwenye sanduku la kura mjiulize nani anafaa kuwa Rais kupitia hoja hizi tatu, ikiwemo ya Othman kuwa mtu mzalendo, mtii na mwaminifu kwa Wazanzibari.
“Huyu si mwingine, ni Othman ambaye hatafuni maneno katika kusimamia maslahi na haki za Wazanzibari,” amesema Jussa na kuongeza;
“Ndani ya miaka mitano, kwa nyakati tofauti, Othman amekuwa akikemea ufisadi na akitaka wachukuliwe hatua. Huu ndio uwajibikaji, hili si la ACT Wazalendo la watu wote maana dhiki inatukumba wote.”
Jussa amesema mgombea urais wa chama hicho, Othman, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, ni chaguo la uwajibikaji na atakayeiletea heshima Zanzibar.
“Uchaguzi huu ni chaguo la maisha mazuri kwa Wazanzibari, sio kikundi cha watu. Tunakwenda kuueleza maana ya uchaguzi huu kwa kiongozi anayepigania maisha ya Wazanzibari, si kikundi cha watu wachache.
“Miaka mitano hii, kila mtu alikuwa analalamika, si mkulima, mfanyabiashara wala bodaboda, kila mwananchi analalamika njaa, ajira na maisha magumu,” amesema Jussa.
Othman atainua uchumi Zanzibar
Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, Juma Duni Haji ‘Babu Duni’, amesema mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ndiye kiongozi sahihi atakayeleta mabadiliko ya kuinua uchumi wa Wazanzibari.
Amefafanua kuwa kwa mazingira ya sasa, Zanzibar inahitaji mabadiliko yatakayowezesha wananchi wa visiwa hivyo kumudu milo mitatu kwa siku.
“Kinachohitaji kwa sasa ni mabadiliko yaliyosubiriwa kwa muda mrefu, mtaani kuna ugumu wa maisha, kila mtu analalamika njaa… tuamue tukampigie kura zote Othman Masoud ndiye atakayetutoa hapa tulipo,” amesema Babu Duni, ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa ACT Wazalendo.