Kocha CBE asepa na somo CECAFA

KOCHA wa CBE, Birhanu Gizaw amesema msimu huu haukuwa mzuri kwa upande wao wakikutana na ushindani mkubwa kwenye mashindano ya CECAFA ya kuwania kufuzu ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.

Mabingwa hao watetezi wa CECAFA waliishia katika hatua ya makundi baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi B, wakianza kwa kupoteza 2-1 dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda na mechi ya mwisho ya kundi kutoa suluhu dhidi ya Top Girls.

Gizaw alisema kilichowaangusha msimu huu ni kwamba hawakuwa na maandalizi mazuri, hasa kwenye eneo la usajili ambalo halikufanyiwa kazi mapema.

Aliongeza kuwa wameondolewa kwenye mashindano lakini hawajaondoka patupu, kuna kitu wamejifunza na wanakwenda kufanyia kazi ili msimu ujao wafanye vizuri.

“Hatukufanya vizuri katika mashindano haya, lakini tumepata mafunzo muhimu. Tutarudi, tujiandae vyema, na tutarejea tukiwa na nguvu zaidi msimu ujao,” alisema Gizaw na kuongeza:

“Msimu uliopita wachezaji wengi waliondoka na hatukuweza kuziba mapengo yao. Tunarudi kurekebisha kwa sababu bado tuna muda wa kufanya hivyo, tumepata uzoefu mkubwa.”

Licha ya kutoridhishwa na matokeo ya timu hiyo, kocha huyo alisema ana imani kuwa makosa yaliyojitokeza yatatumika kama sehemu ya mabadiliko msimu ujao.

Miongoni mwa wachezaji waliokuwa mhimili mkubwa wa timu hiyo, Aregash Kalsa na Ariet Udong walitimkia Yanga Princess, huku mfungaji bora wa timu hiyo, Loza Abera, akisajiliwa China.

Tangu mashindano ya CECAFA yaanzishwe 2021, CBE ina rekodi ya kuwa timu ya kwanza kucheza fainali tatu kati ya tano.

Mara ya kwanza ilicheza mwaka 2021 ikapoteza mbele ya Vihiga Queens, mwaka 2023 ikapoteza mbele ya JKT Queens, na mwaka jana ikatawazwa mabingwa dhidi ya Police Kenya Bullets.