Kocha Minziro aibukia Bigman | Mwanaspoti

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Bigman, Fredy Felix ‘Minziro’, amerejea tena kukifundisha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa 2025-2026, wa Ligi ya Championship, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Zubery Katwila aliyejiunga na Geita Gold.

Minziro aliyewahi kuzifundisha Geita Gold na Tanzania Prisons, aliifundisha Bigman msimu wa 2024-2025, ingawa aliondoka Oktoba 17, 2024 na kujiunga na Pamba Jiji, akichukua nafasi ya Mserbia Goran Kopunovic aliyeondoka pia Oktoba 16, 2024.

Akizungumza na Mwanaspoti, Rais wa Bigman, Ahmed Waziri Gao alisema wamefikia uamuzi wa kumrejesha Minziro kutokana na uwezo wake, hivyo, mashabiki wa kikosi hicho wawe na matumaini makubwa katika Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026.

“Minziro hapa ni nyumbani kwake na hata akiondoka muda wowote anaweza akarudi, baada ya kuondoka Katwila mashabiki zetu walikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua ni kocha yupi tutamleta hivyo, niwaambie watarajie mambo mazuri,” alisema Gao.

Aidha, Gao alisema baada ya kumrejesha Minziro wamehakikisha wanampa mahitaji yake yote muhimu, ili kwa pamoja watimize pia malengo ya kikosi hicho kupanda Ligi Kuu Bara, licha ya ushindani mkubwa uliopo Ligi ya Champioship.

Kwa msimu wa 2024-2025, Katwila aliiwezesha Bigman kumaliza ikiwa nafasi ya nane katika Ligi ya Championship na pointi 47, baada ya kushinda mechi 12, sare 11 na kupoteza saba, ikifunga mabao 29 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21.