Dar wa Salaam. Katika malezi ya mtoto, wazazi wengi hujielekeza zaidi kwenye elimu, nidhamu na maadili, huku wakisahau jambo moja la msingi ambalo ni la kumpatia lishe bora.
Mara nyingi, tabia ya mtoto inapobadilika au kutokuwa ya kuridhisha, mzazi hukimbilia kulaumu mazingira ya shule, marafiki au hata vipindi vya runinga na wengine hudandia hoja ya utandawazi.
Lakini je, mzazi ni mara ngapi umewahi kujiuliza ni kwa kiasi gani chakula anachokula mtoto wako kinaathiri mwenendo wake wa makuzi?
Wataalamu wa malezi na makuzi ya mtoto kwenye baadhi ya kazi zao za kitafiti wanasema wazi kwamba lishe ni zaidi ya chakula cha kushibisha.
Baadhi wanasema lishe bora ni chanzo cha nguvu, afya ya mwili na akili, pia ni msingi muhimu wa tabia njema kwa mtoto.
Uhusiano kati ya aina ya chakula anachokula mtoto na tabia yake ni mkubwa kuliko wengi wanavyodhani.
Joyce Kusekwa mtaalamu wa lishe anasema mtoto anayekula chakula chenye virutubisho vya kutosha ikiwamo protini, madini, vitamini, na mafuta mazuri, huwa na uwezo mzuri wa kufikiri, kuzingatia na hata kushirikiana vyema na wengine.
Anasema watoto hawa mara nyingi huwa watulivu, wachangamfu na wenye nidhamu nzuri shuleni na nyumbani.
Utafiti pia unaonesha kuwa watoto wanaopata kifungua kinywa kila siku huonyesha utulivu zaidi darasani, hupunguza migogoro na walimu na huwa na uwezo wa juu wa kujifunza.
Kwa upande mwingine, watoto wanaokosa lishe bora huathirika kiafya na kiakili, hali ambayo hujidhihirisha kupitia tabia zao.
“Lishe duni, hasa ile yenye sukari nyingi, vinywaji vya kusindikwa viwandani na vyakula vyenye kemikali na rangi bandia, huongeza uwezekano wa mtoto kuwa na msisimko wa kupita kiasi hatulii, anakuwa na hasira za mara kwa mara na hushindwa kujizuia,” anasema George Kapungu, Daktari bingwa wa watoto anayefanya kazi katika hospitali moja jijini Dar es Salaam.
Dk Kapungu anasema hali hiyo inaweza kumfanya mtoto akapata matatizo ya kinidhamu awapo nyumbani na hata shuleni.
Hivyo, wazazi ni vema mkatambua kwamba, lishe ni sehemu ya malezi yenu. Kwa wale ambao mlikuwa hamlifahamu hilo, ni vema mkafahamu kuwa malezi bora hayawezi kutenganishwa na lishe bora.
Mnapojitahidi kuwafundisha watoto heshima, bidii na maadili, ni lazima pia muwahimize kwenye ulaji wa chakula chenye virutubisho vyote muhimu.
Mtoto hawezi kuwa mtulivu na mwenye bidii ya kujifunza iwapo mwili wake hauna nguvu wala ubongo wake hauna lishe ya kutosha kufanya kazi vizuri.
Wazazi wengi hudhani kuwapa watoto vitu kama pipi na juisi za viwandani na zilizoongezewa rangi za chakula ni kuwafurahisha.
Huko ni kuwahatarishia afya na tabia. Ni kwa wazazi kuanza kubadili mtazamo huo kwa kuwaelimisha watoto juu ya umuhimu wa kula chakula safi, salama na chenye virutubisho.
Moja ya njia bora ya kuwalea watoto katika misingi ya lishe bora ni pamoja na kula nao pamoja. Familia zinapokaa pamoja mezani si tu kunawasaidia watoto kula vizuri kwa nidhamu, bali pia hujenga ukaribu na mawasiliano. Katika mazingira haya, mzazi hupata nafasi ya kujua mtoto anakula nini, kwa kiasi gani na namna anavyojihisi.
Aidha, kushirikisha watoto kwenye maandalizi ya chakula huwasaidia pia kufahamu thamani ya lishe bora, kuwajengea heshima ya chakula, na kuwafanya wawe na uhusiano mzuri na vyakula vyenye afya.
Na wazazi mkumbuke kuwa tabia hizi hujengwa taratibu, lakini matokeo yake hudumu maisha yote.
Lishe bora haimaanishi eti utumie gharama kubwa, la hasha! Wazazi wengine hujitoa kwenye jukumu la kutoa lishe bora kwa kisingizio cha ugumu wa maisha au gharama. Ukweli ni kwamba lishe bora haimaanishi kula vyakula vya bei ya juu.
Vyakula vya kawaida kama mboga za majani, maharage, viazi, mihogo, matunda ya msimu, samaki wa mtoni au ziwani na nafaka zisizokobolewa vinaweza kutosha kabisa kutoa virutubisho muhimu kwa ukuaji bora wa mtoto.
Kinachohitajika ni maarifa, kupanga vizuri mlo wa familia na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima kwa vyakula visivyo na virutubishi.
Badala ya kutumia fedha nyingi kununua vinywaji baridi na vitafunwa vyenye sukari, wazazi wanaweza kuwekeza kwenye vyakula vya asili na kujifunza mapishi.
Hivyo, ni vema kila mmoja akatambua kuwa lishe bora ni msingi wa afya, akili na tabia njema ya mtoto.
Mtoto anapokosa chakula bora, si mwili tu unaoathirika bali pia mwenendo wake, uwezo wa kujifunza na hata uhusiano wake na watu wengine.
Mzazi kabla ya kumlaumu mtoto wako kwa ukaidi au kutotii, jiulize kwanza; Je, mtoto wangu anakula vizuri? Je, napanga mlo wa familia yangu kwa kuzingatia virutubisho?
Je, ninakuwa mfano wa ulaji bora?
Tukumbuke lishe bora si jambo la hiyari tena, ni sehemu ya msingi ya malezi. Tukiwalea watoto wetu katika msingi wa chakula chenye afya, tutakuwa tumejenga jamii ya baadaye yenye akili timamu, miili imara na tabia njema.