Maandalizi duni yaiangusha JKU | Mwanaspoti

ALIYEKUWA kocha msaidizi wa JKU Princess, Noah Kanyanga amesema maandalizi hafifu yamechangia timu hiyo kutofanya vizuri kwenye mashindano ya CECAFA kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya JKU kuondolewa kwenye mashindano, rasmi sasa Kanyanga anarudi kwenye majukumu yake ya kocha mkuu Fountain Gate Princess. Mabingwa hao wa Zanzibar walimuazima ili aongeze nguvu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kanyanga alisema timu haikuandaliwa vyema, haikupata mechi za kirafiki kujipima namna gani inakwenda kwenye mashindano hayo.

Aliongeza kuwa mbali na hilo, mabinti hao wanapaswa kujengwa kiakili kabla ya kwenda kushiriki mashindano ya CECAFA ambayo ni makubwa kwa ukanda huu.

“Kuna mambo mengi nimejifunza, kwanza kuandaa timu kwa wakati na kupata muda wa mechi nyingi za kirafiki. JKU imecheza lakini haijapata hata mechi ya kujipima. Unaona kuna wachezaji kibao wameazimwa kutoka Bara,” alisema Kanyanga na kuongeza:

“Pili, kuwa na muda wa kutathmini wapinzani unaenda kukutana nao, na tatu, kwa timu kama hizi zenye vijana wadogo ni kuwajenga kisaikolojia kuwa wanaenda mashindano ya aina gani na sio madogo.”

JKU iliyokuwa katika Kundi C kwenye michuano hiyo na iliondolewa katika hatua ya makundi baada ya kupokea vichapo mfululizo dhidi ya JKT Queens 5-0 na 4-2 kutoka kwa Yei Joints ya Sudan Kusini.