Macho yote kwa Vicky michuano ya NCBA

VIWANJA vya Gofu vya Muthaiga vilivyopo jijini Nairobi, Kenya ndivyo vitaamua nani anastahili kuutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki wa NCBA baada ya kutamatika kwa mashimo 18 majuma machache yajayo.

Tanzania, tayari imeshapata washiriki wakiongozwa na Malkia wa Swing, Vicky Elias kutoka jijini Dar es Salaam.

Vicky pamoja na Madina Idd na Neema Olomi wa Arusha wamekuwa wakifanya vizuri katika viwanja vya Kenya, safari hii atakuwa na watu wengine kabisa katika safari nzito ya kuviteka viwanja hivyo, ambako fainali kuu za michuano hiyo zitafanyika Novemba 28, mwaka huu.

“Nimekuwa maarufu zaidi nje ya Tanzania kuliko viwanja vya nyumbani baada ya kulijengea jina langu vizuri Kenya, Uganda na Afrika ya Kusini,” alisema Vicky.

Baada ya michuano ya kufuzu iliyofanyika Tanzania, Kenya na Uganda, wachezaji watatu bora kutoka kila nchi walifuzu na kukata tiketi za kucheza fainal.

Vicky alifanya vizuri katika mchuano wa kufuzu kwenye viwanja vya TPDF Lugalo mwishoni mwa mwezi uliopita na atakuwa pamoja na Nsajigwa Mwansasu aliyeshinda taji la Gross kwa wanaume baada ya kupiga mikwaju 77 na watatu ni Khalid Shemndolwa, aliyeshinda taji la Divisheni A  akiwa na wastani mzuri wa mikwaju 71.

Vicky ambaye mwaka jana alishiriki katika michuano ya viwanja saba Ukanda wa Pwani ya Kenya na kumaliza nafasi ya tatu, alisema ameanza kujiandaa kwa fainali hiyo akiamini atafanya vizuri.

“Sidhani kama yatakuwa na upinzani mkali kama yale ya Kenya Ladies Open kwa vile si mabingwa wote wanaoshiriki,” alisema na kuwataka Watanzania wamuunge mkono ili aipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Vicky alitwaa tiketi ya kucheza fainali hizo baada kushinda taji la Gross kwa upande  wa wanawake akiwa amepiga mikwaju 74 na tangu kuasisiwa kwake mwaka 2022, michuano hiyo imekuwa ni kati ya mashindano makubwa ya gofu kwa Afrika Mashariki kwa kuwa imekuwa ikiwaweka pamoja wacheza gofu nyota kutoka Kenya, Tanzania na Uganda.