Marekani kurudisha miradi ya USAID Tanzania

Arusha. Ubalozi wa Marekani nchini umethibitisha kuwa miradi ya maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) itarejeshwa, licha ya shirika hilo kufungwa mapema mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili, Septemba 14, 2025, na Balozi wa muda wa Marekani nchini, Andrew Lentz, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Arusha baada ya kumaliza ziara yake katika mikoa ya kanda ya kaskazini.

Balozi Lentz amesema kufungwa kwa USAID hakumaanishi mwisho wa miradi ya maendeleo, bali kutakuwepo na mfumo mpya wa utekelezaji ili kuhakikisha miradi hiyo inaendelea.

Amebainisha kuwa Marekani itashirikiana na mashirika mbalimbali na jamii za wenyeji kuchukua jukumu la kusimamia baadhi ya miradi iliyokuwa chini ya USAID.

“Tutahakikisha miradi inafanyika tena kwa kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa. Lengo letu ni kuendeleza jitihada za uhifadhi na maendeleo ya kijamii,” amesema.

Miongoni mwa miradi iliyopewa kipaumbele ni urejeshaji wa korido za wanyamapori, ambazo ni muhimu kwa mtiririko wa ikolojia. Tanzania ina jumla ya korido 61 za wanyamapori, nyingi zikiwa zimeharibika au kuzibwa kutokana na shughuli za kibinadamu.

Kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili uliokuwa ukifadhiliwa na USAID, juhudi za kuzifungua korido hizo zilianza kwa ushirikiano na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wengine wa uhifadhi.

Awali, USAID ilizindua mradi wa uhifadhi wenye thamani ya Dola milioni 30.5 za Marekani (zaidi ya Sh75 bilioni) mwaka 2022, uliopangwa kutekelezwa kwa miaka mitano hadi mwaka 2026, kwa lengo la kukabiliana na changamoto zinazotishia uhamaji wa wanyamapori na kuhifadhi bayoanuai.

Hata hivyo, mradi huo pamoja na mingine mingi ulisitishwa mapema mwaka huu chini ya utawala wa Rais Donald Trump.

Mbali na sekta ya uhifadhi, USAID iliwahi kutoa zaidi ya Dola milioni 400 kusaidia kuimarisha biashara, kukuza ajira na kuharakisha maendeleo ya Tanzania.

Vilevile, Shirika la Fedha la Maendeleo la Marekani (DFC) lilitangaza mkopo wa zaidi ya Dola milioni 300 kwa Benki ya CRDB mwaka 2024, uliokusudiwa kusaidia zaidi ya biashara ndogo 4,500.

Aidha, DFC na USAID kwa pamoja walitoa dhamana ya mikopo ya ziada yenye thamani ya Dola milioni 52 kwa Benki za Amana na CRDB, fedha ambazo zilielekezwa katika sekta za elimu, uchumi usio rasmi, kilimo, biashara za wanawake na vijana pamoja na afya.

Miongoni mwa wadau wa uhifadhi, shirika la World Wildlife Fund (WWF) limeeleza matumaini kuwa hatua ya kurejesha miradi hiyo inaweza kwenda sambamba na urejeo wa ufadhili kupitia Shirika la Changamoto ya Milenia la Marekani (MCC).