Dodoma. Mgombea ubunge wa Mtumba, Anthony Mavunde amesema kukopa bila elimu ya ujasiriamali na fedha ni chanzo cha mikopo umiza.
Kutokana na hilo, amewataka wananchi hasa kinamama na vijana kuacha kukopa kwa kuiga kwani watajikuta wameingia mahali penye hasara kubwa.
Mavunde ametoa kauli hiyo jana Jumamosi Septemba 13,2025 kwa nyakati tofauti alipokuwa kwenye ziara ya kampeni za mtaa kwa mtaa Kata ya Nzuguni.
Waziri huyo wa Madini amesisitiza watu waache kukopa kabla ya kujua kwa nini wanataka kukopa na jinsi gani wakopaji watanufaika na mikopo hiyo.

Mavunde kwenye harakati za kuomba kura Kata ya Nzuguni
Amesema katika uongozi wake atajitahidi kuwaunganisha kinamama na taasisi za fedha, lakini kabla ya kukopeshwa muhimu watulie kwanza.
“Hata sasa naomba msiingie kichwa kichwa kwenye mikopo na mambo ya kausha damu, subirini kwanza tuwasaidie mpate elimu ya ujasiriamali na fedha ambayo ni nguzo kuu na Siri ya mafanikio,” amesema Mavunde.
Katika hatua nyingine Mavunde ameahidi kuanza ujenzi wa zahanati katika eneo la Mtaa wa Nzuguni A kwa kutambua ukubwa wa kata hiyo.

Kuhusu migogoro ya ardhi amesema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deo Ndejembi au Naibu wake watafika Mtaa wa Mahomanyika wakati wowote kumaliza migogoro ambayo wamekuwa nayo wananchi kwa muda sasa.
Mavunde anagombea Jimbo la Mtumba ambalo ni jipya lililozaliwa kutoka Jimbo la Dodoma Mjini aliloliongoza kwa vipindi viwili mfululizo.
Mgombea nafasi ya udiwani kata hiyo, Leonard Ndama amesema atapambana kusimamia ahadi za mbunge lakini suala la maji ni muhimu akasimama kidete kwani haiwezekani maji yamechimbwa Nzuguni na yanatoka kwa wingi halafu wananchi hawana maji.

Ndama amesisitiza kuongeza madarasa ya shule kwani shule za kata hiyo zinaonekana kuelemewa kwa idadi kubwa ya wanafunzi.