Morogoro. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimewaomba wakazi wa Kata ya Mafisa, Manispaa ya Morogoro, kura katika uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza kwenye kampeni za nyumba kwa nyumba Septemba 14, mgombea udiwani wa Chaumma, Kata ya Mafisa, Gredo Method, amesema wananchi wanapaswa kutoa kura zao kwa wagombea wa chama chake ili kuleta mabadiliko yanayohitajika.
Gredo amesema kuwa viongozi waliomaliza muda wao katika ngazi ya ubunge na udiwani wameshindwa kushughulikia matatizo ya wananchi, hasa kero ya Mto Morogoro ulioacha njia yake ya asili na maji kuingia katika makazi ya watu pindi mvua kubwa zinaponyesha milima ya Uluguru.
“Kata ya Mafisa inahitaji diwani mwenye hoja na msimamo atakayepigania barabara za lami, kufungua njia mpya za kuunganisha maeneo jirani ya Tungi na Kihonda na kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki za kijamii,” amesema Gredo.
Baadhi ya wananchi wamesema matarajio yao katika uchaguzi mkuu, huku Sophia Mapunda (28) mkazi wa Manispaa ya Morogoro, akisema wanahitaji viongozi waadilifu na wachapakazi.
“Madiwani na wabunge wanaochaguliwa wanapaswa kuanza na changamoto zilizopo kwenye mitaa na kata. Wananchi wakipata maendeleo watakuwa na imani na kura zao,” amesema Sophia.
Getruda Edward (49) amesema mfumo wa huduma za afya ni miongoni mwa maeneo yanayoumiza wananchi.
Getruda amesema kuna vituo vya afya na hospitali huwatoza wagonjwa kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000 ili kumuona daktari akiita huo ni mzigo mkubwa.
“Tunahitaji viongozi watakaobadilisha mfumo huu na kuhakikisha barabara za manispaa zinatengenezwa kwa kiwango cha lami badala ya kuachwa za vumbi,” amesema Getruda
Mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kupitia Chaumma, Elizeus Rwegasira amewataka wananchi kujitokeza kusikiliza sera na ilani ya chama hicho.
Rwegasira amesema sera hizo zinaainisha changamoto zinazokabili wananchi na kutoa njia mbadala za kuzitatua kwa ngazi ya urais, ubunge na udiwani katika maeneo husika