MGOMBEA URAIS CCM DK.SAMIA AUTAJA KIGOMA KAMA MKOA WA KIMKAKATI KIUCHUMI,BIASHARA

*Aelezea hatua kwa hatua yanayokwenda kufanyika Kigoma miaka mitano ijayo

*Maelfu ya wananchi wampa Vibe la maana alipokuwa akiomba kura kuelekea Oktoba 29

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Kigoma

MAELFU ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma hasa Kigoma Mjini wamejitokeza kwa wingi katika mkutano wa kampeni wa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ameeleza kwa mipango ya Serikali kwa mkoa huo sio tena Kigoma mwisho wa reli bali ni mkoa wa kimkakati kwa uchumi na biashara.

Akihutubiwa wananchi waliofurika katika Uwanja wa Katosho uliopo Kata ya Kibirizi Jimbo la Kigoma Mjini Dk.Samia Suluhu Hassan ametumia nafasi hiyo kueleza mchango wa mkoa huo kwa ujumla katika maendeleo ya nchi kupiia viongozi wa kitaifa.

“Miaka iliyopita watu walikuwa wamezoea kusema Kigoma ni mwisho wa reli lakini kwa kasi ya maendeleo yanayoonekana sasa mkoa huo ni kitovu cha uchumi na biashara.

“Hata ujenzi wa reli ya SGR haitoshia mkoani Kigoma bali itakwenda hadi Burundi kisha kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hivyo mkoa huo siyo tena mwisho wa reli.

“Agosti mwaka 2022 alifika wilayani Kakonko kuzindua miradi mitatu muhimu ambayo ni barabara ya Kabingo – Nyakanazi, mradi wa maji Nyamfisi na hospitali ya wilaya.”

Amesema kuwa miradi hiyo ni sehemu ya maendeleo ambayo yalianzia katika kipindi cha awamu ya tano kisha yeye akaikamilisha na alipokuwa akizindua miradi hiyo aliahidi hakuna miradi itakayosimama.

“Wakati nilipokuwa Kibondo Oktoba 16 mwaka 2022 nilisisitiza kila tulichokiahidi katika awamu ya tano, tunakwenda kuyafanyiakazi na hakuna kitakachosimama. Kwa haya niliyoyasikia tangu nilipoingia Kigoma kwa hakika hakuna kilichosimama. Ni dhahiri kwamba serikali imetimiza ahadi zake.”

Ametaja miongoni mwa ahadi ambazo CCM na serikali yake iliweka kwa wananchi mkoani Kigoma ni kuutoa mkoa huo kutoka mkoa wa pembezoni hadi kuufanya kuwa mkoa wa kimkakati, jambo ambalo limedhihirika.

Dk.Samia amesisitiza  Kigoma sasa siyo mkoa wa pembezoni bali ni mkoa wa kimkakati.”Siyo mwisho wa reli bali ni kitovu cha biashara na maendeleo. Kwa uwezo wa Mungu tutayakamilisha hayo. 

“Ili kulifikia lengo hilo kwenye miundombinu ya usafiri na safirishaji ambayo ndiyo muhimili mkubwa wa kukuza uchumi, tumejidhatiti kuunganisha mkoa huu kwa njia zote yaani barabara, anga, reli na njia ya maji.

“Tayari maboresho ya uwanja wa ndege yanaendelea, njia tayari imeanza kutumika na jingo linaendelea kujengwa. Mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa kitaifa wa kulifungua anga la Tanzania na kuimarisha shirika letu la ndege la Air Tanzania,” amesema.

Ameongeza kuwa tayari shirika hilo ndege zake zinatua katika mkoa huo huku likiendelea kupanua wigo wa usafirishaji ambapo hivi karibuni linatarajiwa kuanzisha safari za ndege kwenda Lagos, Nigeria.

“Kwasasa serikali inafanya maboresho ya viwanja vya ndege 14 ambavyo sita vimekamilika na vinane ujenzi unaendelea ili kuboresha viwanja hivyo.

Kwa upande wa kuhusu reli amesema Kigoma ni sehemu muhimu ya reli ya SGR kwani kuna vipande ambavyo ni Tabora – Kigoma na kipande cha Uvinza – Msongati.

Amefafanua baada ya reli hiyo kufika Kigoma, itaelekea Burundi kisha kwenda mashariki mwa DRC. “Tumekamilisha sehemu ya kwanza na ya pili Dar es Salaam hadi Dododoma na sehemu zote zilizobakia ya tatu, nne na tano ambayo ni Mwanza – Isaka itakamilika mwaka huu, ya sita ambao ni Tabora – Kigoma na ya saba Uvinza – Msongati, kazi inaendelea.

“Sambamba na SGR tunaiboresha reli iliyopo ya zamani (MGR) kwa kununua vichwa vipya vya treni vitatu, mabehewa mapya 22 ya abiria na mabehewa ya mizigo 44. Vilevile jumla ya mabehewa 350 ya mizigo na 33 ya abiria, tunayafanyia ukarabati na mengi tayari yameshakamilika,” alisisitiza.

Pia amesema kazi hiyo imefanyika kwa kushirikiana na wabia ambao walikarabati mabehewa 68 yanayotunza ubaridi kwa ajili ya kusafirisha mazao ya matunda na mbogamboga.

Dk.Samia aliyekuwa akihitimisha mikutano ya kampeni katika mkoa huo ameeleza serikali imefanya maboresho ya kanuni kuhusu uendeshaji wa huduma kupitia reli na sasa sheria na kanuni zinaruhusu waendeshaji binafsi kufanyabiashara katika miundombinu ya reli iliyowekwa na serikali.

Aidha amesema lengo la hatua hiyo ni kuongeza ufanisi wa usafirishaji mizigo na abiria kuwezesha mzunguko wa kasi kiuchumi.

Kuhusu usafiri wa majini, Mgombea urais Dk.Samia amesema Serikali imetekeleza miradi mikubwa katika maziwa makuu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa bandari, meli za abiria na mizigo.

Amefafanua kwa upande wa Ziwa Tanganyika hususan Mkoa wa Kigoma, serikali inaendeleza ujenzi na ukarabati wa bandari za Ujiji, Kibirizi, Kabwe na Kigoma na bandari ya Kalema iliyopo Katavi na Kasanga iliyopo mkoani Rukwa.

Pia Serikali inajenga meli nne katika bandari ya Kalema ambapo moja imekwisha kamilika huku zingine tatu zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

“Matarajiao meli hizi zitakapokamilika zitahudumia Tanzania na nchi Jirani za DRC, Zambia na Burundi. Mwaka jana tulianza kukarabati na uboreshaji meli kongwe za Mv Liemba ambayo tunatarajia kuikamilisha mwaka ujao wa fedha.

“Tunapokwenda mbele na mkitupa ridhaa yenu, tutakuwa na mradi mwingine mkubwa wa kuunganisha reli na usafiri wa meli ambapo tayari tumesaini mikataba mitatu ya ujenzi wa kiwanda cha ujenzi wa meli ambao umeshaanza kutekelezwa eneo la Katabe hapa Kigoma. Ujenzi wa meli mbili za mizigo, moja kwa ajili ya Ziwa Tanganyika na nyingine kwa ajili ya Ziwa Victoria.”

“Ya hapa Ziwa Tanganyika itakuwa na uwezo wa kubeba tani 3500 itakayokuwa na ghorofa moja, meli hizo maalum zitapokea shehena ya mizigo inayosafirishwa na reli ya SGR kutoka bandari za Bahari ya Hindi. 

“Hata kama ipo bandari ya Mtwara kwa sababu tumeiweka maalum kwa ajili ya pembejeo za kilimo, tutashusha kule zije Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwa SGR kwenda mikoa mingine.”

“Huo ndiyo mpango wa serikali katika usafirishaji kwa njia ya maji huku akibainisha kuwa miradi hiyo inaendelezwa maeneo mbalimbali nchini ikiwemo bandari ya hindi, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.