MJNUAT kutoa wahitimu wa kwanza mwakani

Butiama. Baada ya kusuasua kwa muda mrefu kuanza kutoa masomo, hatimaye Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT), kilichopo wilayani Butiama Mkoa wa Mara, kinatarajia kuwa na mahafali ya kwanza mwakani.

Chuo hicho kilikaa miaka saba bila kuanza kutoa mafunzo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha.

Akizungumza kwenye kongamano la kisayansi lililofanyika chuoni hapo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mara, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Lesakit Mellau, amesema jumla ya wanafunzi 73 wapo mwaka wa pili chuoni hapo.

Amefafanua kuwa wanafunzi hao wanasoma fani za uchumi kilimo na uchumi biashara pamoja na shahada ya viumbe hai vya majini.

Amesema kwa mwaka huu wa masomo wanatarajia kudahili wanafunzi 1,200 baada ya kukamilika kwa kiasi kikubwa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho.

“Mwaka huu lazima tuwe na udahili wa wanafunzi wengi watakaokuwa wa shahada nne na stashahada tatu, ambapo tunatarajia kila fani itakuwa na wanafunzi si chini ya 150,” amesema Profesa Mellau.

Ametaja fani ambazo wanafunzi hao watachukua kuwa ni pamoja na Teknolojia ya Habari za Biashara, Uvuvi na Ufugaji Samaki, Mazao na Uzalishaji, Sayansi ya Afya ya Wanyama, pamoja na Uchumi kilimo na Biashara Kilimo.

Akizungumza kuhusu kongamano, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dk Masinde Bwire, amesema kamisheni hiyo imeandaa kongamano hilo kwa lengo la kuwakutanisha watafiti, wanasayansi, na wadau kujadili na kutoa mapendekezo mbalimbali juu ya namna ya kulinda Mto Mara kufuatia tafiti zilizofanywa kuhusu mto huo.

Dk Bwire amesema hii ni mara ya nne kwa kamisheni hiyo kuandaa kongamano la aina hiyo na kwamba tayari matokeo chanya yameanza kuonekana, ikiwa ni pamoja na hatua za Serikali ya Kenya kulinda chanzo cha Mto Mara.

“Mto Mara unaanzia katika Milima ya Mau kule Kenya, na pale palikuwa na uharibifu mkubwa sana, lakini baada ya makongamano haya, tayari Serikali ya Kenya imeweka uzio wa umeme ili kuzuia watu kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi,” amesema.

Ameiomba Serikali ya Tanzania kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira na hifadhi ya vyanzo vya maji kwa ukamilifu, hatua ambayo itasaidia ulinzi wa bonde hilo.

“Tanzania kuna ile sheria ya mita 60 bado haijasimamiwa vizuri, ni sheria nzuri ikisimamiwa italeta matokeo mazuri.

“Hadi sasa kuna mafanikio madogo kama vile kupungua kwa mmomonyoko wa udongo, na maeneo oevu sasa yameanza kuwa na hali nzuri,” amesema.

Akifungua kongamano hilo la Sayansi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, ameagiza kuwa pamoja na mambo mengine, kongamano hilo linatakiwa kuandaa andiko la mradi kwa ajili ya usimamizi wa bonde la Mto Mara.

Amesema kutokana na athari zinazoikabili bonde hilo, ipo haja ya wadau kuwa na mipango mikakati mingi kukabiliana na hali hiyo ili changamoto ziweze kupata suluhisho la kudumu.

“Kongamano hili liwe na andiko la mradi, zitafutwe fedha kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali zitakazokuwa na matokeo chanya kuhusu uhifadhi endelevu wa bonde letu,” amesema.

Ameagiza kuwepo kwa ushiriki wa wadau wengi katika kongamano la kisayansi mwakani, akisema makongamano hayo yana mchango mkubwa katika uendelevu wa bonde hilo na yanasaidia kuwajengea maarifa washiriki ili kuja na mipango thabiti ya kupambana na changamoto.

Mzungumzaji mkuu katika kongamano hilo, Dk Musuto Chirangi, amezitaka mamlaka husika kutenga bajeti ya kutosha ili kusaidia kutafsiri matokeo ya tafiti mbalimbali.

“Tunafanya tafiti nyingi, lakini hazitafsiriwi kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo ukosefu wa fedha. Hizi tafiti zina umuhimu mkubwa, zikitumika vema zinaweza kuleta matokeo chanya katika jamii zetu,” amesema.