Babati. Mgombea udiwani wa kata ya Magara, wilayani Babati Mkoa wa Manyara, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Gonzalez Mkoma, amewaomba wakazi wa eneo hilo kumpa kura nyingi za ndiyo ili apambane na changamoto zinazowakabili.
Baadhi ya changamoto zinazowakabili wakazi wa kata hiyo ni ukosefu wa kituo cha afya, ukosefu wa nishati ya umeme katika baadhi ya vitongoji na upungufu wa huduma ya maji.
Mkoma amesema atahakikisha kero na changamoto za huduma ya maji katika eneo hilo zinapambanuliwa ili jamii ipate maji.
Amesema kilio cha wananchi wa eneo hilo, zaidi ya 22,000, cha kupata kituo cha afya atalifanyia kazi, kwani huduma za afya wanazipata katika zahanati ya kijiji cha Magara.
Akizungumza kuhusu nishati ya umeme, amesema atafuatilia ili vitongoji ambavyo havina huduma hiyo viweze kufungiwa.
“Ili kupunguza ugumu wa maisha, nitahakikisha umeme unafika katika vitongoji vilivyokosa, kwani hata kusaga unga wa mahindi inamlazimu mtu kukodi pikipiki kwa Sh4,000 kwa gharama za kwenda na kurudi,” amesema Mkoma.
Amesema suala la bei ya chini ya mbaazi, ya Sh600 hadi Sh700 kwa kilo, atalibeba ili kuwanyanyua kiuchumi wakulima ambao hivi sasa wameathirika nayo.
“Baadhi ya wakulima wanachungia mifugo mbaazi shambani kutokana na kukosa bei kubwa ya kununua, nitabeba hilo ili wakulima wafaidike na mbaazi,” amesema Mkoma.
Amesema suala la barabara ya lami, kilomita 20 kutoka Mbuyu wa Mjerumani hadi Magara na kilomita 34 hadi Mbulu, jumla kilomita 54, atambana mbunge ili ijengwe kwa lami.
Amesema ujenzi wa barabara hiyo upo kwenye utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM 2025-2030, hivyo atambana mbunge wakumbushe wizara ili ijengwe kwa lami.
“Nawaomba wakazi wa Magara wanipe kura za kutosha, wawachague mgombea ubunge, Daniel Sillo na urais, Samia Suluhu Hassan, ili tutatue changamoto hizo kwa kushirikiana kwa pamoja,” amesema Mkoma.
Mkazi wa kata ya Magara, Mwanaisha Adam, amesema ana matarajio kuwa Mkoma atapambana na changamoto za eneo hilo pindi akichaguliwa.
“Hata kama hana mpinzani wa chama kingine, Mkoma ambaye ni mgombea wa CCM anapendwa na wana Magara kwani amekuwa akijitolea kwenye mambo ya kijamii kabla ya kuomba udiwani,” amesema Mwanaisha