Mwakwama CUF ataja vipaumbele vitano Uyole

Mbeya. Mgombea Ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Mwakwama, ametaja vipaumbele vitano ambavyo atavifanyia kazi iwapo atachaguliwa, huku akisisitiza uongozi shirikishi na kulaani vitendo vya utekaji.

Akihutubia wananchi leo Jumapili Septemba 14, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uyole Junction, Mwakwama amwsema ili jimbo hilo liwe la mfano, mshikamano unatakiwa kuanzia ngazi ya familia.

Ameahidi kuwa iwapo atashinda, hatakubali kushikilia nafasi zinazomuweka mbali na wananchi kama vile urais wa mabunge duniani (IPU), badala yake jukumu lake litakuwa kuwatumikia wananchi waliompigia kura.

“Ninasikitika kuona watoto wakifukuzwa shule kwa kukosa ada. Nikichaguliwa, nitasimamia ada zote za wanafunzi na pia nitajenga stendi kubwa ya kisasa hapa Uyole,” amesema Mwakwama.

Ameahidi kupigania jimbo hilo kupata Halmashauri, kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi na wakati wote kuwa karibu na jamii kutatua kero zao.

Pia amesema hataenda bungeni kupiga meza au makofi bali kupigania soko la kisasa la mazao, ikizingatiwa kilimo ndicho shughuli kuu ya wananchi wa Uyole.

Aidha, Mwakwama ameahidi kushughulikia changamoto ya maji safi, hasa kwa shule za msingi na sekondari, na kupiga marufuku tabia ya kurekodi au kutangaza misaada inayotolewa kwa wahitaji akieleza kuwa inawadhalilisha wananchi.

Awali, Katibu wa CUF Mbeya Mjini, Ayoub Hinjo aliwataka wananchi wasifanye makosa kuchagua wagombea wa CCM akidai chama hicho kimeshindwa, na sasa ni wakati wa CUF kushika dola.

Amesema iwapo mgombea urais wa chama hicho, Gombo Samandito, atashinda, hatua ya kwanza itakuwa kuanzisha mchakato wa katiba mpya na kumuachia huru Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini.

Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa wa CUF, Rose Kahoji, amesisitiza sera za chama hicho ikiwemo elimu bure isiyo na gharama, huduma bora za afya na kupunguza udumavu kwa watoto.

Amekosoa CCM kwa kushindwa kuboresha huduma licha ya muda mrefu madarakani na kuwataka wananchi kutumia kura zao Oktoba 29 kuleta mabadiliko.