SD Eibar ya Ligi ya Wanawake Hispania imeboresha eneo la ushambuliaji kwa ajili ya msimu huu ikimsajili nyota wa Kitanzania, Opah Clement ambaye ana rekodi nzuri Ulaya.
Opah kabla ya kujiunga na timu hiyo msimu uliopita aliichezea FC Juarez ya Mexico lakini hakuwa na msimu mzuri alicheza mechi sita bila kufunga bao wala asisti.
Lakini kabla ya Juarez aliitumikia Henan Jianye ya China akafunga mabao matano, Kayseri Kadin mabao matano na Besiktas ya Uturuki sita, huku Simba Queens ambako ndiko alikoanzia maisha ya soka la kulipwa akifunga mabao 34 msimu 2021/22.
Opah anajiunga na timu hiyo ambayo imekuwa na changamoto kwenye eneo la washambuliaji tangu msimu uliopita na msimu huu zimeendelea kuonekana baada ya kucheza mechi mbili bila washambuliaji wake kufunga bao.
Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi na katika mechi 30 ilishinda 10, sare nane na kupoteza 12 ikifunga mabao 24 na kuruhusu 41.
Kwenye mabao 24 yaliyofungwa msimu uliopita 10 pekee yamewekwa kambani na washambuliaji, huku mengine yakifungwa na viungo na mabeki, tatizo ambalo pengine ujio wa Opah atalitatua kutokana na rekodi yake alikopita.
Mbali na kasi yake, uwezo wake wa kufunga mabao kwenye nafasi ngumu na kutengeneza nafasi unaweza kuleta matumaini kwa timu hiyo.
Uwezo wake wa kucheza kama mshambuliaji wa kati au winga unampa faida ya kuwa mchezaji mwenye matumizi mengi kikosini.
Mshambuliaji wa timu hiyo, Hapsatou Malado Diallo (Senegal) msimu uliopita alifunga mabao matatu huku Ane Campos aliyetimkia Athletic Club ndiye alikuwa mshambuliaji mwenye mabao mengi akifunga saba.