Akizungumza katika kikao hicho cha kitaifa, Kamishna Mkuu wa PST, Dkt. Meshack Stanley Chiburwa, alisema kuna baadhi ya watu wasio na nia njema wamekuwa wakiwalaghai vijana kwa zawadi ndogo ili wawatumie kufanya vitendo vya uhalifu.
“Niwaase vijana wetu wa Kitanzania, kuna watu hawana dhamira njema wanawatumia kwa zawadi ndogo ndogo kisha kuwapotosha ili kujiunga kwenye machafuko. Kuondoa amani kwenye taifa kuna gharama kubwa kujenga tena. Msikubali kutumika kama chambo,” alisema Dkt. Meshack.
Dkt. Meshack alieleza kuwa taasisi yake tayari imeanza kutekeleza kampeni hizo kwa makundi mbalimbali ikiwemo bodaboda, akisisitiza kuwa kundi hilo lina nguvu kubwa katika jamii na linahitaji kupewa uelewa wa kutokuhusiana na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.
Aidha, aliiomba Serikali kuhakikisha haki inatendeka kila inapostahili, jambo linalosaidia kuondoa mvurugano unaoweza kuathiri amani.
“Vyama vya siasa navyo lazima vihakikishe sera zinazowanadiwa kwa wananchi zinamkomboa Mtanzania na kuzingatia haki, kwani ndilo hitaji kubwa la watu wanaowachagua,” aliongeza.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi (Mstaafu) Barnabas Mwakalukwa alisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa wazalendo, hususan wakati wa uchaguzi:
“Wananchi tuwe wazalendo. Tusiingize nchi kwenye machafuko kwa kuvunja katiba. Tuipende nchi yetu, hatuna nyingine zaidi ya hii,” alisema.
Naye, Kamishna Msaidizi wa PST, Bi. Upendo Clement Mkunde, aliongeza kuwa wamekusudia kulenga zaidi kundi la vijana kwani ni rahisi kubadilishwa kimtazamo na kuachana na njia mbaya za kutumia vurugu kupata wanachotaka.