Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka mafundi mkoani humo kuhakikisha kazi zao zinakuwa na ubora unaokidhi ushindani wa soko kwa kutumia teknolojia za kisasa na nyenzo bora.
Akizungumza leo Septemba 14, 2025, wakati wa kongamano la mafundi lililoandaliwa na kampuni ya Magic Builders, James amesema mafundi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.
Amesisitiza kuwa mafundi wanaposhirikiana na viwanda vya ndani kupitia matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini, wanasaidia kukuza uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
“Tunapovipa thamani viwanda vya wazawa, tunapanua mzunguko wa fedha na kuongeza ajira kwa vijana wetu. Hii ndiyo njia ya kuhakikisha kila mmoja ananufaika,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Vilevile, amewataka wahandisi mkoani Iringa wanaoshiriki katika miradi ya ujenzi kuhakikisha bidhaa za ndani zinapewa nafasi kwenye majengo ya Serikali na ya sekta binafsi.
Amesema Serikaliimewekeza katika miradi mingi ya ujenzi, ambayo kwa sehemu kubwa inatekelezwa na vijana. Amesema hali hiyo imechangia kuongeza kipato cha kaya na kuinua uchumi wa wananchi.
Katika hatua nyingine, James ameeleza kuwa ubora na ustawi wa kampuni za ndani ni uthibitisho kuwa sera za Serikali zinalenga maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Magic Builders Foundation, David Barongo, amesema ipo haja ya mafundi kupewa hadhi zaidi kwa kurasimishwa ili kuongeza ufanisi na maslahi yao.
Barongo amebainisha kuwa kampuni yake, ambayo ni ya kizawa, imeendelea kujitanua kimataifa kwa kusafirisha bidhaa zake katika nchi za Zambia, Zimbabwe, Kenya, Congo na nchi nyinginezo.
“Niseme tu kwamba kampuni hii imejipanga kuwapa mafundi motisha kwa kuanzisha bima za afya, kwani tunataka mafundi wajione ni sehemu ya familia kubwa ya Magic Builders,” amesema.
Kwa upande wake, mlezi wa kampuni hiyo na mfanyabiashara wa rangi mkoani Iringa, Mohamed Abri, amewahimiza wakandarasi na wafanyabiashara kutumia bidhaa za ndani ili kuboresha huduma zao na kukuza uchumi wa wazawa.
“Ni vyema kampuni au Serikali inapopata tenda kubwa za ujenzi, itumie mafundi wa ndani ya mkoa wa Iringa badala ya kuwaleta mafundi kutoka maeneo mengine kama Dar es Salaam,” amesema Abri.
Sultani Mapunda, mmoja wa mafundi wa Iringa, amesema semina hiyo imeonesha namna Serikali inavyowakumbuka na kuwajali mafundi katika kuhakikisha wanaendelea kutengeneza vitu vyenye ubora.
“Hii kwetu ni fahari kubwa na niombe tu Serikali kuwa semina kama hizi ziwe endelevu ili kuongeza maarifa na ubunifu kwa mafundi,” amesema Mapunda.
Naye fundi Sostenes Sanga ameongeza kuwa bidhaa zinazozalishwa Tanzania zina ubora wa hali ya juu na zinachangia kuongeza tija kwenye kazi zao za kila siku, hivyo mafundi wakipewa nafasi ya kutumia bidhaa hizo wataendelea kuthamini viwanda vya ndani na kushirikiana katika kukuza uchumi wa Taifa.