Ndoa ni muunganiko rasmi wa watu wawili wanaopendana, kwa lengo la kuishi pamoja kwa upendo, heshima, na mshikamano.
Kikawaida, ndoa hufanyika kwa uwazi na kushuhudiwa na familia, jamii na mamlaka husika kama taasisi za dini au serikali.
Hata hivyo, uzoefu hivi sasa unaonyesha, kuna ongezeko la ndoa zinazofungwa kwa siri, yaani, ndoa ambazo hufanyika kwa usiri mkubwa bila wanandoa kuwahusisha ndugu, marafiki, jamaa au hata wenza kwa wale waliokwishaoa.
Mkazi huyu wa mkoani Dar es Salaam anasema alishawahi kuoa mke kwa siri na akaishi naye kwa zaidi ya mwaka bila mkewe wa kwanza kung’amua. Anasimulia:”Kiukweli mke wangu wa kwanza naweza kusema ni bomba na najua hata wanaume wengine walimtamani. Ila migogoro yangu naye ilinisababisha nitafute mahala pa kupumulia.
Miongoni kwa mambo yaliyonichukiza kwake ni kujali zaidi ajira yake kuliko upendo kwa mumewe na hata familia. Ilifikia hatua hata kukutana kimwili ilikuwa kwa kubembeleza mno. Hakutaka kuwajibika kimwili kwangu.
‘’Kuona hivyo nikaona isiwe tabu, nikatafuta mwanamke pembeni ambaye hakuwa mchepuko bali tulifunga ndoa kabisa tena ya kidini.
Uzuri wangu mimi nilimficha tu mke wangu, lakini ndugu wa karibu na wazazi wangu walijua.”
Kwa nini watu hufunga ndoa hizi? Wataalamu wanataja sababu kadhaa ikiwamo kukwepa vikwazo vya kijamii au dini.
Kwa mfano, katika baadhi ya jamii, ndoa kati ya watu wa dini tofauti, kabila tofauti au tabaka tofauti hukataliwa vikali. Ili kudumisha mapenzi yao, wenza huamua kufunga ndoa kwa siri bila taarifa kwa familia zao.
Sababu nyingine wanaume wanaotaka kuoa wake wa pili mara nyingi hufanya hivyo kwa siri ili kuepuka migogoro na wake wa kwanza au jamii ambayo haikubali ndoa za wake wengi.
Hali kadhalika, wanawake wengine huolewa na wanaume wenye wake bila kujua, na baadaye huamua kuendelea kuwa wake wa siri kwa sababu ya mapenzi au ahadi walizopewa.
Pia wapo wanaoogopa kuwa familia zao hazitakubali chaguo lao la mpenzi kutokana na sababu mbalimbali kama tofauti za kielimu, kipato, au historia ya maisha ya mwenza.
Ili kuepuka kukataliwa au mizozo, wanachukua hatua ya kufunga ndoa kwa siri.Wengine wanaweza kuwa na matatizo ya kifamilia kama migogoro, mirathi au kutengwa.
Hali hizi huwafanya wasiwe na uhusiano mzuri na familia zao, hivyo kuamua kufunga ndoa bila kushirikisha ndugu. Wengine huogopa gharama za harusi na sherehe, hivyo kuamua kufanya ndoa ya siri isiyohitaji matumizi makubwa.
Kwa wale watu maarufu kama wafanyabiashara, viongozi wa kisiasa na wa Serikali na wengineo, huamua kuficha ndoa zao kwa sababu ya kulinda heshima, sifa au kuepuka kashfa.
Mtu anaweza kuona kuwa ndoa itaharibu taswira yake mbele ya jamii au itahatarisha nafasi yake kazini au kwenye ulingo wa kisiasa.
Sababu nyingine inawahusu wapenzi wa muda mrefu wanaoamua kuhalalisha uhusiano wao kwa ndoa ya siri, hasa pale ambapo mmoja wao tayari yupo kwenye ndoa nyingine.
Wanaweza kuona ni njia ya kuendelea na uhusiano wao kwa namna “halali” kisheria au kidini, bila kuathiri ndoa zao za awali.
Ingawa ndoa za siri zinaweza kuonekana kuwa suluhisho la muda kwa baadhi ya watu, zinaweza kusababisha changamoto nyingi za kijamii, kisaikolojia na kisheria.
Ndoa ambazo hazijasajiliwa au kushuhudiwa na mamlaka husika mara nyingi hukosa nguvu ya kisheria. Hii inamaanisha kuwa mke au mume hawezi kudai haki zake za ndoa, urithi au matunzo pale mume/mke anapofariki au pale ndoa inapovunjika.
Mwenza wa ndoa ya siri anaweza kujihisi kutothaminiwa, kutengwa, au kufichwa. Hii huweza kusababisha maumivu ya moyo, wasiwasi, na hata msongo wa mawazo kwa muda mrefu.
Ndoa za siri zikigundulika baada ya muda, husababisha migogoro mikubwa ya kifamilia na kijamii. Familia huhisi kudharauliwa, marafiki hukosa imani, na watoto wanaozaliwa kwenye ndoa hiyo wanaweza wasikubaliwe kijamii.
Pia watu wanaofunga ndoa kwa siri huonekana kama wasio waaminifu, wanaoficha mambo, au wenye tabia ya kisiri. Hali hii huathiri uhusiano wao na jamii na hata taaluma au kazi zao.
Ndoa ya siri mara nyingi haina msingi imara wa kijamii unaowezesha kusaidiana na kushikamana. Wanandoa hushindwa kusaidiana katika nyanja mbalimbali kwa sababu hawawezi kutangaza hadharani kuwa wameoana.
Athari kwa watoto.Watoto wanaozaliwa kwenye ndoa za siri hukumbana na changamoto ya kukosekana kwa uthibitisho wa wazazi wao, haki ya urithi, na hata kupigwa chapa ya ubaguzi kijamii. Wengine hukua wakihisi kutengwa au kutothaminiwa.
Je, tushabikie ndoa hizi?
Swali hili halina jibu rahisi, kwani linategemea muktadha wa kila ndoa. Hata hivyo, kwa ujumla, ndoa ya siri si suluhisho bora la muda mrefu katika uhusiano wa kimapenzi.
Faida chache za ndoa hizi kama kuepuka migogoro ya familia au jamii au kuepuka gharama kubwa za sherehe, ni za manufaa ya muda mfupi tu.
Ndoa ya siri haina usalama wa kisheria, haina baraka za familia, na mara nyingi hujengwa juu ya woga na wasiwasi. Hii husababisha uhusiano usiokuwa na amani, imani, wala mwelekeo.
Katika hali ya kawaida, ndoa ya siri kwa maoni ya baadhi ya watu, haifai kwani hujenga msingi wa kutoaminiana, ukosefu wa uwazi na kukosa heshima kwa taasisi ya ndoa.
Hata hivyo, kama kuna sababu maalum zinazowalazimu watu kufunga ndoa za siri, basi inashauriwa kuwa ni kwa muda na kwamba hatua zichukuliwe mapema kuifanya ndoa hiyo iwe ya wazi na halali kwa jamii.
Ndoa sio uhalifu ni jambo jema na ndio maana hata katika baadhi ya dini, tendo hilo linachukuliwa kama ibada.
Ndoa ni muungano unaohitaji uwazi, heshima na uhalali wa kijamii na kisheria. Ingawa baadhi ya watu wana sababu zao binafsi za kufunga ndoa kwa siri, athari zake kwa mtu binafsi, mwenzi wake, watoto na jamii kwa ujumla ni kubwa.
Badala ya kukimbilia ndoa ya siri, ni vyema kutafuta njia za mawasiliano, suluhisho la migogoro, na ushauri nasaha ili kujenga ndoa zenye afya na imani.
Kwa hivyo, jamii inapaswa kuelimishwa zaidi juu ya madhara ya ndoa za siri, huku pia taasisi za kijamii na kidini zikihamasisha vijana kuoa na kuolewa kwa uwazi, kwa baraka za familia na jamii.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi, anasema ndoa si jambo la siri, na ndio maana hutangazwa.
” Ni lazima itangazwe na siku 21 zipite ili kama kuna mtu anayejua chochote kuhusiana na hao watu wanaofunga ndoa watoe taarifa.
Hata hivyo, anasema ikiwa wahusika hawana kizuizi na kwa sababu ya mazingira fulanifulani, wanaweza wakapewa ruhusa waende kufunga ndoa ya siri mahali fulani.
“Lakini huo siyo utaratibu wa kawaida mtu anatoka tu anaomba nifunge ndoa ya haraka haraka…hakuna cha ndoa ya haraka haraka hapa, lazima tuchunguze tujue kama wewe hauna vizuizi au vipi. Kwahiyo hilo unalozungumza la ndoa za siri ni mahala ambapo sasa hata taratibu za ndoa hazipo, yaani watu wanafungisha kama mchezo wa kuigiza,” anafafanua na kuonya kuwa ndoa za aina hiyo sio za kushabikia.
Kwa upande wake, Juma Nkumilwa, Imam wa Msikiti wa Jihad Nyahanga Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, anasema ndoa hizo zimekithiri huku akibainisha kuwa zipo zinazokubalika kisheria na zisizokubalika.
” Ile inayoweza kukubalika kisheria ni ile ndoa ambayo imefuata taratibu na misingi yote ya sheria, kwahiyo hawajaibana hawa bali huyu mwanamke tayari mawalii zake wamemuozesha’ anasema na kuongeza kuwa ndoa batili ni ile watu wanaozeshwa pasina kufuatwa kwa vigezo vilivyowekwa kidini.
Anasema katika Uislam mafundisho yanataka wachumba kuficha uchumba lakini watangaze ndoa.
” Suala la kuchumbiwa fulani ni mambo ya kifamilia kwahiyo familia ndiyo inajua kwamba binti yetu amechumbiwa na fulani lakini suala la ndoa linatakiwa litangazwe. Itangazwe ifahamike kuwa fulani ameoa na ziko hekima nyingi za kutangaza ndoa’ anaeleza.