Kigoma. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuja na mradi wa kuunganisha usafiri wa reli na meli katika kusafirisha mizigo kutoka bandari zilizopo Bahari ya Hindi, kisha kusafirishwa kwa treni ya kisasa (SGR) kwenda mikoa ya bara.
Pia, amesema wataendelea na uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji wa barabara, majini, reli na angani ili kuwa na usafiri wa uhakika utakaochochea shughuli za kiuchumi.
Samia amebainisha hayo leo Septemba 14, 2025 wakati wa mkutano wake wa kilele wa kampeni katika Mkoa wa Kigoma ambapo awali alitembelea majimbo ya Uvinza, Kasulu na Buhigwe, kabla ya kuhitimisha Kigoma mjini.
Akieleza mikakati yake baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, mgombea huyo amesema watakuja na mradi wa kuunganisha usafiri wa meli na wa treni ili kuharakisha na kurahisisha usafirishaji wa mizigo.
Amesisitiza kwamba, tayari hatua za awali kuelekea jambo hilo zimefanyika huku akisema mradi huo utakuwa na matokeo makubwa pindi utakapokamilika na utachochea uchumi wa Taifa hili.
“Mkitupa ridhaa yenu, tutakuwa na mradi mwingine wa kuunganisha reli na usafiri wa meli. Tayari tumesaini mikataba mitatu ya ujenzi wa kiwanda cha ujenzi wa meli ambao umeanza kutekelezwa eneo la Katabe hapa Kigoma; na ujenzi wa meli mbili, moja kwa ajili ya Ziwa Tanganyika na nyingine kwa ajili ya Ziwa Victoria,” amesema Samia.
Mgombea huyo ameongeza kuwa meli itakayokuwa Ziwa Tanganyika itakuwa na uwezo wa kubeba tani 3,500 na itakuwa ya ghorofa mbili na inatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo katika ziwa hilo.
“Meli hizi maalumu zitapokea shehena za mizigo zinazosafirishwa na reli ya SGR kutoka bandari za Bahari ya Hindi kwa maana ya bandari za Dar es Salaam na Mtwara.
“Mzigo kutoka Mtwara utashusha Dar es Salaam, kisha utasafirishwa kwa SGR kutoka Dar kuja Kigoma. Kwa hiyo, huo ndiyo mpango wetu,” amesema Samia huku wananchi wakimshangilia.
Mgombea huyo amesema Serikali yake itaendelea na ukarabati wa meli kongwe ikiwamo ya Mv Liemba ili ziendelee kutoa huduma kwa wananchi zikisaidiana na meli mpya zinazojengwa.
Samia amesema katika Ziwa Tanganyika, wanaendelea na ukarabati wa bandari za Ujiji, Kibirizi na Kabwe (Kigoma), Karema (Katavi) na Kasanga (Rukwa). Amesema wanajenga meli nne kwenye bandari ya Karema, moja imekamilika na nyingine tatu ziko katika hatua mbalimbali.
“Matarajio yetu ni kwamba meli hizi zitakapokamilika, zitahudumia pia nchi jirani za Burundi, Zambia na Jamhuriya Kidemokrasia ya Congo (DRC),” amesema Samia kwenye mkutano huo.
Kuendelea kumtumia Dk Mpango
Wakati huohuo, Samia ameahidi kuendelea kumtumia Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango katika shughuli mbalimbali kwa yale yaliyo mbele yake baada ya kuchaguliwa.
Dk Mpango aliyeteuliwa na Samia mwaka 2021 baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitangaza kustaafu katika nafasi hiyo ili apate muda wa kupumzika.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Samia aliwashukuru wananchi wa Kigoma kwa kumtoa Dk Mpango kwani amemsaidia kazi zake nyingi na kwamba ni kiongozi mwadilifu na mzalendo.
“Dk Mpango amekuwa kiongozi mtiifu, mwadilifu, mchapakazi na mzalendo nafasi zote alizowahi kushika. Kwa kweli amenisaidia sana katika kipindi cha miaka minne iliyopita, amekuwa sehemu ya mafanikio yaliyopatikana.
“Nataka niwaambie, Dk Mpango bado ataendelea kutusaidia kama sehemu ya kutekeleza yanayokuja mbele yetu pindi mkitupa ridhaa yenu. Hongereni sana wana Kigoma kwa kuleta watu wanaoweza kulitumikia Taifa hili,” amesema Samia.
Mbali na nafasi ya Makamu wa Rais, Dk Mpango aliwahi kutumikia kama Waziri wa Fedha na Mipango na pia Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango wakati wa Serikali ya awamu ya nne.
Wagombea ubunge wafunguka
Mgombea ubunge wa Kigoma mjini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, amesema Serikali ya Samia imefanya mambo magumu ambayo hayakuwahi kufanyika huko nyuma hasa katika upatikanaji wa maji, kwani Kigoma walikuwa wanayaona maji kwenye Ziwa Tanganyika lakini majumbani kwao hawana maji, lakini leo hali ni tofauti, maji yanapatikana.
Pia, amesema amefanya kazi kubwa ya kuunganisha mkoa huo katika gridi ya Taifa, jambo ambalo halikuwezekana huko nyuma lakini yeye amelifanikisha ndani ya kipindi kifupi.
“Tuna mfupa mwingine mgumu ambao tunaamini utaufanya, tunaomba barabara za lami ndani ya mji wetu, ukitupa hata kilomita 75, tutakushukuru sana,” amesema mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi wa Kigoma mjini.
Baba Levo amemshukuru Samia kwa dhamira yake ya kuufanya Mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara na anaendelea na ukarabati na ujenzi wa meli katika Ziwa Tanganyika, amesema atakwenda kuwahimiza makandarasi wa meli hizo ili wamalize haraka zianze kutoa huduma.
Mgombea ubunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba amesema Samia ametekeleza ahadi aliyoitoa wakati anaingia madarakani kwamba anakwenda kuifungua nchi.
Amesema katika kipindi chake, makusanyo ya mapato yameongezeka, Bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri na matokeo yake nchi inakusanya mapato ya kutosha na ufanisi katika bandari hiyo ni mzuri.
“Ulipoingia, tulikuwa tunapokea watalii 600,000, lakini ulipocheza filamu ya Royal Tour, sasa tunapokea watalii milioni mbili. Matokeo yake, mapato yameongezeka zaidi na kusaidia katika utoaji wa huduma za kijamii,” amesema mgombea huyo.
Ameongeza kuwa Serikali ya Samia inajenga meli tatu katika Ziwa Tanganyika na amekuja na dhamira ya kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa ziwa hilo, jambo litakalowezesha kufanya biashara na nchi jirani za Burundi na DRC.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa viti maalumu, Zainabu Katimba amesema katika kipindi cha miaka minne, Samia amepeleka Sh11.4 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Kigoma.
Amesema wanaiona dhamira yake ya kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, ndiyo maana anajenga meli tatu katika ziwa hilo zitakazorahisisha biashara katika ukanda huo.
“Dhamira yako tunaiona kupitia miradi ya maendeleo. Tunaona unajenga reli ya kisasa katika mkoa wetu itakayotuunganisha na Burundi, hii ni kazi kubwa itakayoufungua mkoa huu,” amesema Katimba.
Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kumpigia kura mgombea huyo wa urais, ashinde kwa kishindo, aendelee kuleta maendeleo katika mkoa huo.
Mgombea ubunge wa Muhambwe, Florence Samizi amesema katika jimbo lake, vituo vya afya vimefikia saba kutoka vitatu alivyovikita huku akijenga shule mpya sita na zahanati sita.
Amesema mgombea huyo wa urais ameboresha huduma za afya kwani amepunguza vifo vya mama na mtoto kutoka 506 kwa kila vizazi hai 100,000, hadi kufikia vifo 104, jambo ambalo amesema limemfanya atunukiwe tuzo ya kimataifa ya Bill and Melinda Gates.
“Katika miaka yake minne, ameonesha uwezo wake wa kutekeleza mambo magumu ambayo hayakufanywa na viongozi wengine waliomtangulia. Twendeni tukampigie kura nyingi ili aendelee kuliongoza Taifa hili kwa mara nyingine,” amesema Samizi.