Sh300 milioni za Baps kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea msaada wa Sh250 milioni kutoka Taasisi ya Baps Charities kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na ununuzi wa vifaa tiba muhimu.

Msaada huo umekabidhiwa leo Jumapili, Septemba 14, 2025, katika hafla iliyofanyika hospitalini hapo jijini Dar es Salaam.

Uongozi wa JKCI umepongeza hatua hiyo na kuueleza kuwa si msaada wa kifedha pekee, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika maisha ya Watanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, amesema msaada huo umekuja wakati bado kuna changamoto kubwa kwa watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo, lakini hawana uwezo wa kugharamia matibabu.

“Nashukuru kwa msaada huu. Utasaidia kununua vifaa tiba na pia kutoa mafunzo kwa madaktari wetu. Huu ni mchango wa moja kwa moja kwa maisha ya watoto wetu. Tunatoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono juhudi hizi,” amesema Dk Kisenge.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia JKCI imepanga kutoa huduma za upasuaji kwa watoto 141 ifikapo mwisho wa mwaka huu. Kati ya huduma hizo, asilimia 70 zitagharamiwa na Serikali huku asilimia 30 iliyobaki ikitegemea msaada kutoka kwa wadau na wahisani.

Kwa upande wake, Mratibu wa Baps Charities Tanzania, Kapil Dave, amesema msaada huo ni mwendelezo wa jitihada zilizoanza mwaka 2015, kufuatia maono ya marehemu Shubash Patel, mmoja wa waanzilishi wa taasisi hiyo na mdau mkubwa wa JKCI.

“Tumekabidhi Sh250 milioni kwa ajili ya watoto wenye matatizo ya moyo. Tunatambua kuwa gharama za matibabu ni kubwa kwa familia nyingi, hivyo hii ni njia yetu ya kuchangia pale panapohitajika msaada wa dharura,” amesema Dave.

Aidha, Dave amesifu kiwango cha huduma kinachotolewa na madaktari wa JKCI, akibainisha kuwa uwepo wa taasisi hiyo umeondoa ulazima wa wagonjwa kusafirishwa nje ya nchi kutafuta matibabu, hali iliyopunguza gharama kwa serikali na familia.

Katika hatua nyingine, Baps Charities pia imekabidhi Sh50 milioni kwa Taasisi ya Tumaini la Maisha kwa ajili ya kusaidia watoto wanaougua saratani. Fedha hizo zinalenga kugharamia matibabu na mahitaji ya kitabibu kwa watoto kutoka familia zisizo na uwezo.