Katika dunia ya sasa talaka haimaanishi tena mgawanyiko usiokwepeka hasa linapokuja suala la malezi.
Kimsingi, mbali ya talaka, wazazi waliotalakiana wanapaswa kukumbatia mtazamo wa kisasa wa kushirikiana katika kulea watoto wao, hata kama wanaishi tofauti.
Kwa miaka mingi, talaka ilihusishwa na ratiba ngumu za ulezi, mapambano ya kisheria, na mawasiliano ya migogoro. Lakini sasa, familia nyingi zinabadilisha simulizi ya maisha baada ya talaka. Wanachagua ushirikiano badala ya ugomvi, na kujenga ushirikiano wa kulea watoto unaoweka maslahi ya mtoto mbele.
“Niliwahi kufikiria kwamba talaka itamaanisha mwisho wa familia yetu,” anasema Musa Saidi, baba wa watoto wawili wa jijini Dar es Salaam
Anaongeza: “Lakini sasa najua ilikuwa mwanzo wa sura mpya. Hatujaoana tena, lakini bado ni wazazi pamoja. Hilo halibadiliki.”
Kutoka migogoro hadi ushirikiano
Mfumo wa ulezi wa pamoja umebadilika. Badala ya mtazamo wa “mshindi na aliyeshindwa” katika malezi, wazazi sasa wanaandaa mipango inayobadilika na kuzingatia mahitaji ya mtoto.
Baadhi hutumia kalenda za pamoja na programu maalum kupanga ratiba, matukio ya shule, na miadi ya matibabu. Wengine huishi karibu karibu au hata kwenye nyumba moja kwa zamu, m
ambapo watoto hubaki nyumbani na wazazi hubadilishana rariba ya kuishi nao.
Lisa na James, wazazi wa pamoja kutoka mkoani Arusha, wanaeleza mpangilio wao kama “ushirikiano wa makusudi.”
“Tunaongea kila siku kuhusu watoto, tunagawana gharama kwa usawa, na hata kuhudhuria mikutano ya walimu pamoja,” anasema Lisa. “Sio rahisi kila wakati, lakini inafanya kazi kwa sababu tunawaweka watoto mbele,” Anaongeza.
Zana za kidijitali zimekuwa msaada mkubwa. Programu kama OurFamilyWizard, Cozi, na TalkingParents husaidia kupunguza mawasiliano ya kimigogoro, kurekodi matumizi ya kifedha, na kufuatilia ratiba za ulezi.
Baadhi zinajumuisha huduma za upatanisho mtandaoni, zinazorahisisha kutatua migogoro bila kurudi mahakamani.
“Teknolojia imeondoa msongo mwingi katika kupanga mambo. Inafanya kila kitu kuwa wazi na kinachoeleweka,” anasema James.
Licha ya mafanikio haya, ulezi wa pamoja una changamoto zake. Maumivu ya kihisia kutokana na talaka yanaweza kuwa makubwa, hasa ikiwa mgawanyiko ulihusisha usaliti au ugomvi mkubwa. Familia zilizochanganyika (blended families) pia huleta ugumu katika kupanga ratiba na mitazamo tofauti ya malezi inayoweza kuchochea mvutano.
Daktari wa saikolojia ya watoto, Dk Rose Aluko, anaonya: “Ulezi wa pamoja wenye mafanikio unahitaji ukomavu wa kihisia, mawasiliano ya mara kwa mara, na zaidi ya yote, dhamira ya pamoja ya kutanguliza maslahi ya mtoto. Bila hayo, hata zana bora haziwezi kusaidia.”
Watoto wanasemaje kuhusu mipangilio hii mipya? Tafiti zinaonyesha kuwa watoto hunufaika wanapoweka uhusiano mzuri na kila mzazi. Uwepo wa wote wawili, uthabiti wa kanuni na ratiba, na kuepuka migogoro ya wazazi ni vitu vinavyotabiri ustawi wa kihisia wa mtoto.
“Watoto hawahitaji wazazi wakamilifu. Wanahitaji wazazi waliopo,”anasema Dk Aluko.
Mahakama za familia katika mataifa mengi zinaanza kuakisi mabadiliko haya. Majaji wengi sasa wanahimiza malezi ya pamoja na mgawanyo sawa wa muda wa mtoto, ikiwa hali ni salama na inayowezekana.
Mafunzo ya ulezi, ambayo hapo awali yalikuwa hiari, sasa yanakuwa ya lazima kwa wanandoa wanaoachana ili kuwasaidia kushirikiana vizuri katika kulea.
Kadri mitazamo ya kijamii inavyobadilika, ndivyo pia dhana ya familia inavyoendelea kubadilika. Uso mpya wa ulezi wa pamoja ni wenye kubadilika, unaohusisha hisia, na unaomlenga mtoto. Unajengwa si kwa chuki, bali kwa uwajibikaji na upendo wa pamoja kwa mtoto.
“Huenda tusiwe wanandoa tena, lakini bado tuko pamoja kwa ajili ya watoto wetu. Kwa kweli, wanafaidika zaidi kwa hali hii,” anasema Maria Stambuli Mkazi wa Morogoro.