Dar es Salaam. Ikiwa kesho, Septemba 15, dunia itaadhimisha Siku ya Demokrasia, wadau wa siasa nchini wameibuka na mitazamo tofauti juu ya hali ya demokrasia Tanzania, baadhi wakisema imeimarika na wengine wakidai bado zipo dosari.
Wamedai dosari hizo zinahitaji meza ya mazungumzo na kupendekeza yafanyike baada ya uchaguzi wa mkuu wa Rais, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Wanaosema demokrasia imeimarika nchini, kigezo wanachotumia ni fursa ya vyama vingi kushiriki uchaguzi na kuwepo kwa amani wakati wa mchakato huo. Vyama 18 vya siasa vinashiriki uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, wanaona bado kuna dosari, wakidai baadhi ya matukio kama ya wagombea kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi, kuminywa kwa uhuru wa kuzungumza na wagombea binafsi kutoruhusiwa kugombea.
Mitazamo hiyo ya wadau inakuja wakati kesho, Septemba 15, dunia itaadhimisha Siku ya Demokrasia, lengo likiwa kukuza na kuendeleza demokrasia katika kila nchi kwa mifumo inayokubalika. Maadhimisho hayo ni baada ya mwaka 2007, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhitaji nchi mbalimbali kuadhimisha siku hiyo kila ifikapo Septemba 15 ya kila mwaka.
Kulingana na Ripoti ya Freedom House ya mwaka 2023, Tanzania ilipata alama 32 kati ya 100 katika kipimo cha uhuru. Nchi hupimwa kulingana na uhuru wa kisiasa na kiraia, na kwa mujibu wa takwimu hizo, Tanzania imetafsiriwa kuwa nchi isiyo huru.
Hali hiyo inaashiria changamoto katika maeneo kama uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, haki, uhuru na uwazi wa uchaguzi.
Mbali na Freedom House, Ripoti ya Democracy Index ya The Economist Intelligence Unit (EIU) ya mwaka 2022, iliiorodhesha Tanzania kuwa nchi yenye utawala wa mabavu, ikiwa na alama 344 kati ya 100. Hii inaashiria bado kuna vikwazo vinavyoathiri demokrasia ya nchi, hasa katika ushirikishwaji wa kisiasa na utawala wa sheria.
Leo, Septemba 14, 2025, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Mohamed Abdallah, amesema kwa kiasi kidogo Tanzania imepiga hatua kwenye demokrasia lakini haijaendana na kasi ya karne ya sasa.
“Tumeona awamu iliyopita kulikuwa na mambo yaliyozikandamiza demokrasia, ikiwemo kupiga marufuku mikutano ya siasa, Bunge kuonyeshwa mubashara na uchaguzi uliporwa, bado hatujafikia kasi inavyotakiwa,” amesema.
Husna amesema ishara za kuminywa kwa demokrasia, kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, zimeanza kuonekana kwa baadhi ya wagombea kuenguliwa kuanzia ngazi za vyama. Amewataka wananchi kutambua demokrasia haipatikani kupitia mtu mmoja, bali wanapaswa kujitambua na kuwachagua watu wanaowataka.
Mitazamo hiyo inatofautiana na wa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Evaline Munisi, ambaye amesema hali ya demokrasia nchini ni nzuri kwa kuwa hakuna hofu na watu wana uhuru wa kufanya siasa bila kutishiwa.
“Hayo yote yanaonesha uimara wa demokrasia yetu, tunashiriki uchaguzi katika mazingira ya amani. Demokrasia ndio msingi wa taifa letu, tunapaswa kuitunza amani yetu,” amesema Munisi.
Mwanaharakati wa masuala ya kisiasa, Dk Ananilea Nkya, amesema kama tafasiri ya demokrasia ni utawala wa watu lakini wakati huu wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, hali ni tofauti.
“Demokrasia nchini haipo vyema, mwaka huu wa uchaguzi ni maalumu kwa wananchi kumtafuta kiongozi kupitia sanduku la kura, lakini mchakato mkubwa unanzia kwenye vyama vya siasa vyenyewe kwa kutafuta viongozi bora,” amesema na kuongeza;
“Mfano nafasi ya urais, kila chama kilipaswa kutumia mchakato wa ndani kupata mgombea ambao wananchi watakuja kumpigia kura, mwaka huu hakuna chama kimeendesha mchakato wa kushindanisha watu wake kupata kiongozi atakayekuja kupigiwa kura na wananchi,”amesema.
Amesema wakati wa maadhimisho ya siku ya demokrasia duniani, vyama vya siasa vimewaangusha wananchi kupata viongozi kwa mfumo wa demokrasia.
“Demokrasia kwenye vyama haipo vizuri, kwa hiyo hatuwezi kuutarajia uchaguzi huu utupe viongozi wanaowajibika kwa wananchi,” amesisitiza Dk Nkya
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa ngome ya Vijana wa chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo, amesema ili demokrasia ionekane nchini, haihitaji tu kutajwa kwenye katiba, bali misingi yake itekelezwe.
Amesema mfumo wa demokrasia hauwezi kuwa imara kama mifumo ya taasisi na sheria haijatekelezwa vizuri.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba, amesema hali ya demokrasia bado haipo sawa.
“Jaji Francis Nyalali angekuwepo sasa angeumia, kwani vuguvugu na matamanio ya Watanzania angeangalia kwenye mikutano ya 1992 hadi 1993. Tunaweza kusema tuna demokrasia ambayo haijakomaa sana, tupo 1982,” amesema.
Kibamba amesema demokrasia hupimwa kwa watu kutoa sauti zao bila hofu, kuchangamana bila vikwazo vyovyote, haki ya mtu kwenda atakako bila kuzuiwa. Amesisitiza kuwa kuna mambo hayana taswira nzuri nchini.
Pia kuna sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019 yenye mlolongo mkubwa wa kuzuia taasisi au mashirika binafsi kutoa elimu ya masuala ya siasa.
Eneo lingine ambalo Kibamba anasema ni Tanzania kwa kuwa ni nchi ya demokrasia ilipaswa mtu asiye na chama cha siasa aruhusiwe kugombea bila kupata vikwazo vyovyote.
“Hadi mwaka 2015 Tanzania tulipiga hatua kwenye masuala ya demokrasia, watu walikuwa huru kusema. Tunapaswa kufanya nini baada ya kipindi hiki cha uchaguzi ni kurudi kujitafakari upya, kuanzisha mazungumzo ya kitaifa ya ujenzi wa demokrasia na kuondoa mazingira yaliyopo sasa,” amesema Kibamba.