::::::::::::
14 Septemba 2025, ARUSHA
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimeandaa mafunzo
yatakayowakutanisha Wafanyakazi na Waajiri yanayojulikana kama “Semina ya Waajiri
na Viongozi wa Matawi ya TUGHE yatakayofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 15-18 Septemba 2025.
Mafunzo hayo muhimu yanatarajia kuwakutanisha takribani washiriki 1000 kutoka kutoka
Serikalini na Taasisi za Serikali na Binafsi ambapo walengwa wakuu ni pamoja na Wakuu
wa Taasisi (Mamlaka za Ajira), Wakuu wa Idara, Viongozi wa Matawi ya TUGHE, Wawakilishi wa Makundi Maalum, Makatibu wa Afya/Matron/MOI/DMO/RMO, Maafisa
Ustawi wa Jamii, Wanasheria na Maafisa Uhusiano wa Taasisi, Makatibu na Makatibu
Wasaidizi wa Mabaraza ya Wafanyakazi.
Akielezea maandalizi ya tukio hilo muhimu kwa Waajiri na Wafanyakazi, Katibu Mkuu wa
TUGHE, *Cde. Hery Mkunda* amesema kuwa maandalizi yanakwenda vizuri yapo katika hatua za kuhitimisha kuelekea siku ya Ufunguzi ambapo washiriki kutoka sehemu mbalimbali Nchini wameshaanza kuwasili Jijini Arusha.
Aidha katika hatua nyingine Cde. Mkunda amebainisha katika siku za mafunzo mada mbalimbali zitawasilishwa na wakufunzi wabobezi katika masuala tofauti tofauti kama
vile Nafasi ya Akili mnemba/Artificial Intelligence (AI) na teknolojia za kidigitali katika
kuimarisha afya na usalama kazini,Taratibu za uendeshaji wa mashauri ya Watumishi wa
Umma, Usuluhishi na Uamuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi dhidi ya Waajiri, Kazi
na huduma zitolewazo na vyama vya Wafanyakazi.
“Sisi TUGHE ambao ndiyo waratibu wa mafunzo haya tumejipanga kikamilifu kuhakikisha
malengo ya kuanzishwa kwa mafunzo haya yanatimia. Tunawashukuru sana Waajiri
pamoja na Wafanyakazi kwa mwitiko mkubwa mlioonesha katika kujiandikisha kushiriki
mafunzo haya” Cde. Mkunda
Katika taarifa yake Cde. Mkunda ameeleza kuwa mafunzo hayo yatahitimishwa kwa
washiriki wote kupata fursa ya kutembelea katika Kivutio Kikubwa cha Mlima mrefu kuliko
wote barani Afrika, Mlima Kilimanjaro. Ziara hii itakwenda sambamba na kuhitimisha
mafunzo haya kufanya shughuli mbalimbali kama vile kupanda mlima, kugawa vyeti kwa
washiriki, kula na kunywa pamoja na kufurahi.
Mafunzo haya yanayojulikana kwa jina la Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya
TUGHE yalianza kutolewa rasmi mwaka 2018 hadi leo jumla ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE wapatao 4500 wamepata mafunzo huku idadi ya washiriki imekuwa
ikiongezeka kila mwaka na hitaji la mafunzo haya linazidi kuongezeka.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO KWA UMMA -TUGHE