Dar/ mikoani. Kampeni si lelemama ndivyo unaweza kuelezea kile kinachotokea kwa baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani kushindwa kufanya mikutano ya kampeni, huku suala la ukata likitajwa kuwa miongoni mwa sababu za tatizo hilo.
Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), ndicho pekee katika vyama vya upinzani kinachoonekana kufanya mikutano kwa kuzingatia ratiba iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) huku baadhi havijafanya hata uzinduzi.
Hii inafanya baadhi ya wananchi wavichukulie baadhi ya vyama vya upinzani kuwa ni vya msimu, havikujipanga.
Hali inatokea wakati tayari ratiba ya kampeni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani iliyoanza Agosti 28, 2025 ifikie robo ya kwanza, huku baadhi ya vyama hivyo vikidai vinafanya mikutano ya kampeni kwa kadri vitakapopata rasilimali fedha.
Kusuasua huko haiishii kwenye kampeni za urais pekee, hali iko hivyo pia katika kampeni za nafasi za ubunge na udiwani kwa wagombea wa vyama hivyo huku Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwa kimeshafanya mikutano katika mikoa tisa nchini.
Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa Union for Multiparty Democracy (UMD), Moshi Kigundula amesema ukata unawalazimu kuacha baadhi ya siku zipite bila mikutano ya kampeni.
Kigundula ameeleza wangetamani kufanya kila mkutano kwa mujibu wa ratiba lakini hawana rasilimali ikiwamo fedha kugharamia kampeni, hivyo wanajivutavuta na kufanya mikutano kwa kuzingatia uhalisia wa kiasi cha fedha walichonacho.
“Tumeshafanya mikutano mitatu hadi sasa na leo (jana) tupo Tanga hapa kwa ajili ya mkutano. Hatuwezi kufanya kila siku, kwa sababu hatuna fedha. Tunafanya mikutano pale tunapomudu,” amesema mtendaji mkuu huyo wa UMD.
Kwa sababu ya ukata, amesema wameshindwa kutofautisha misafara ya mgombea urais na mgombea mwenza, wameamua wote wawe katika msafara mmoja.
“Huo msuli tunatoa wapi? Hatuna fedha ya kusema mgombea urais aende kule na mgombea mwenza huku, tunajivutavuta. Kwa hiyo wote wanakwenda sehemu moja tunafanya tukimaliza tunajikusanya tunafanya kwingine,” amesisitiza.
Hali inayofanana na hiyo, inakikabili pia Chama cha NCCR-Mageuzi ambacho hadi sasa hakijazindua kampeni za urais.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Avelyn Munisi amesema uzinduzi utafanyika leo, Septemba 14 2025, mkoani Kigoma.
Katika ufafanuzi wake kuhusu sababu ya kuchelewa kuzindua, amesema kwanza ni mkakati wa chama hicho, lakini ukata ni jambo lingine lililosababisha hali hiyo.
“Sisi ambao hatuna ruzuku wala vitega uchumi tunajitegemea wenyewe kwa kila kitu, lazima tuwe na ukata. Lakini hata vyama vikubwa navyo vinakabiliwa na ukata. Ni bora kuchelewa kuzindua tusije tukaanza mapema na kuishia njiani.”
“Tunataka kuweka heshima ya NCCR-Mageuzi ile ya mwaka 1995. Ni kweli tumechelewa kuzindua, lakini tutazindua kwa kishindo na kwa sababu ya uchumi, tukizindua kwa kuchelewa tutafika hadi mwisho,” ameeleza Katibu mkuu huyo.
Hata hivyo, amesisitiza kila chama kina mkakati wake na NCCR-Mageuzi, kuchelewa kuzindua kampeni zake ni miongoni mwa mikakati iliyoiweka katika uchaguzi wa mwaka huu.
Kama ilivyo kwa NCCR- Mageuzi na UMD, hata UPDP inakabiliwa na ukata, hali iliyofanya kiandae ratiba yake kwa kutenganisha siku, badala ya kila siku kama inavyoelezwa na Katibu Mkuu wake, Hamadi Mohamed Ibrahim.
Tangu chama hicho kilipozindua kampeni zake Septemba 5, mwaka huu Ibrahim amesema mkutano mwingine imefanyika Septemba 10, Musoma mkoani Mara.
“Ukweli tumeifanya ratiba yetu kuwa hivi kwa sababu ya rasilimali fedha. Kusema ukweli shida kubwa inayotusumbua ni uhaba wa rasilimali fedha,”amesema.
“Tunafanya mikutano ya kampeni kwa kadri hali inavyoturuhusu, hatuna uwezo wa kufanya leo, kesho na keshokutwa, hatuna fedha,” amesema Ibrahim.
Pamoja na uhalisia huo, amesema watahakikisha wanawafikia wapigakura wengi kupitia mikakati mbalimbali, ikiwamo kuwatumia wagombea wa ngazi za chini na viongozi wa chama hicho, mikoa na wilaya katika kufanya kampeni kisayansi.
Baadhi ya wagombea ubunge wa vyama vya upinzani katika Mkoa wa Mbeya, wameiambia Mwananchi kuwa, ukata na ratiba ndio kinachowakwamisha, huku wakiahidi kabla ya muda kuisha tayari watakuwa wameshazindua kampeni hizo.
Mgombea ubunge wa Uyole kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Mwakwama amesema ukata ndio sababu kubwa iliyochelewesha kuanza kampeni, akiahidi kuwa hivi karibuni atafanya hivyo na atawafikia wapiga kura wengi.
“Nilitarajia kuzindua Septemba 14, lakini tarehe hiyo kutakuwa na mgombea urais wa chama cha DP, hivyo hairuhusiwi , natarajia Septemba 19, 2025 lakini kubwa zaidi ni masuala ya fedha yanatatiza,” amesema Mwakwama.
Mgombea huyo amefafanua kuwa, kampeni za chini kwa chini zinaendelea, isipokuwa anaendelea kujipanga kwa ajili ya mkutano wa hadhara, akieleza kuwa mkutano mmoja una gharimu takribani Sh500,000.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo, Malongo Wailes amesema alitarajia kuzindua Septemba 10, lakini walikuwa wanasubiri hatima ya mgombea urais, Luhaga Mpina.
Katibu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Godfrey David amesema pamoja na wagombea wake kutozindua kampeni, lakini bado wapo ndani ya siku 60 zilizoelekezwa na INEC kuhusu kampeni.
“Nina wagombea wawili nafasi za udiwani Mbarali na Kyela, kutofanya kampeni hadi sasa ni suala la maandalizi na bado muda upo, tunafanya mipango kwa ajili shughuli hiyo” amesema David.
Mchambuzi wa siasa jijini Mbeya, Elisha Michael amesema kuchelewa kwa kampeni za wagombea inaweza kuwa ni uchumi wa vyama na kupotea kwa ushindani kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
“Kuna majimbo wagombea ni chama kimoja, lakini unakuta sehemu walipo wapinzani nguvu yao kifedha ni ndogo hali inayofanya mvuto na ushindani wa kisiasa kupotea,” amesema mdau huyo wa siasa.
Imeandikwa na Saddam Sadick (Mbeya), Juma Issihaka na Bakari Kiango (Dar).