Mbeya. Ili kukabiliana na tatizo la upofu unaoepukika, Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Helen Keller International inatarajia kuweka kambi ya siku sita mkoani Songwe kwa ajili ya kuwahudumia wenye tatizo la mtoto wa jicho.
Huduma hiyo inatarajia kuwafikia wananchi 700 katika maeneo mbalimbali mkoani humo, ikiwa na lengo la kuwafikia wananchi waliopo pembezoni, haswa vijijini, ambao watalamu wanakosekana na hawana uwezo wa kufika katika hospitali kubwa kupata huduma hiyo.
Akizungumza leo, Septemba 14, Mratibu wa huduma za macho Mkoa wa Songwe, Dk Jofrey Josephat, amesema huduma hiyo itatolewa bure na wataalamu kutoka Hospitali ya Kanda (MZRH) kwa kushirikiana na Shirika la Helen Keller International.
Amesema huduma hiyo imeanza kutolewa jana, Jumamosi, katika Hospitali ya Wikaya ya Mbozi, akibainisha kuwa matarajio yao ni kuwafikia wananchi takribani 700 kutoka vijijini, wanaosota kupata matibabu kutokana na umbali mrefu na gharama kubwa.
“Kambi hii ya siku 6 inalenga kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la ugonjwa wa mtoto wa jicho Tanzania kwa wananchi wa maeneo ya vijijini ambao wamekuwa waathirika wakubwa kutokana na kukosekana kwa huduma hizo na wataalamu waliobobea katika matibabu haya.
“Tayari huduma imeanza kutolewa na tunatarajia wananchi takribani 700 kutoka vijijini hapa mkoani Songwe watafikiwa. Tumefanya hivi kutokana na kubaini uwapo wa wagonjwa hawa kukosa matibabu kwa sababu gharama za kufuata matibabu ni kubwa,” amesema Dk Josephat.
Mtaalamu huyo amefafanua kuwa visababishi vya ugonjwa wa mtoto wa jicho ni pamoja na umri mkubwa, mtindo wa maisha, au watu wenye kisukari ambao wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huo, pamoja na matumizi ya muda mrefu ya dawa za steroid.
Ameeleza visababishi vingine ni mwanga wa jua, uvutaji sigara, matumizi ya pombe, majeraha ya macho au historia ya familia, akieleza kuwa wenye changamoto hizo wataweza kupata matibabu.
“Wataalamu watatoa ushauri na matibabu kwa wagonjwa. Lengo ni kuhakikisha Tanzania inaishi bila ugonjwa wa mtoto wa jicho. Niwaombe wananchi wajitokeze kwa wingi kwa kipindi hiki ili kupata huduma,” amesema.
Kwa upande wake, Daktari bingwa wa macho katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, Dk Barnabas Mshangila, ameeleza kuwa huduma hiyo ya upasuaji ya mtoto wa jicho inawezesha kurudisha nuru kwa mtu ambaye hakua anaona na kuweza kuona dunia tena.
“Upasuaji huu unachukua muda mfupi na mgonjwa hawezi kuhisi maumivu kwa sababu anapewa dawa ya kuzuia maumivu, na baada ya siku moja kufanyiwa upasuaji, mgonjwa anaweza kuona tena,” amesema Dk. Barnabas.
Meneja Mradi wa Shirika la Kimataifa la Helen Keller, Athumani Tawakali, amesema wanendelea kushirikiana na serikali katika kutoa huduma za upasuaji wa mtoto wa jicho kwa wananchi wa Wilaya ya Songwe.
Pia ameshukuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Mkoa wa Songwe kwa ushirikiano, na ameeleza kuwa mradi huo, unaofadhiliwa na Alcon Foundation, unalenga kuboresha huduma za afya ya macho kwa kurejesha kuona kwa maelfu ya wananchi katika mikoa ya Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali na hospitali hii kwa ujumla katika kuwasaidia wananchi wenye changamoto za afya katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Songwe ili kurejesha afya zao. Wananchi wajitokeze kupata fursa hii,” amesema Tawakali.
Baadhi ya wananchi wilayani humo wamesema uwapo wa huduma hiyo inayotolewa bure ni fursa kwao, wakiishukuru Serikali na wataalamu kuweza kuwafikia, huku wakieleza kuwa hali hiyo imewapa matumaini.
Edward Mkoko amesema wamekuwa wakikutana na changamoto za gharama na mara nyingine kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo, hivyo ujio wa madaktari hao utarejesha matumaini mapya.
“Tunaishukuru Serikali ambayo imegharamia matibabu haya kwa kutuletea nyumbani madaktari. Ni wazi gharama za usafiri na huduma ni kubwa sana ambazo ni ngumu kuzipata. Hii inarejesha matumaini kwetu wagonjwa,” amesema Mkoko.
Naye Ericka Mziho amepongeza huduma bora waliyoipata, akitoa shukrani kwa wataalamu na serikali kwa kuwakumbuka wananchi waliopo vijijini ambao walikosa matibabu hayo kutokana na gharama kubwa.