Canada. Uliwahi kuhusishwa kwenye mgogoro wa ndoa na kuombwa ushauri?
Tunadhani ni wengi wamewahi kufanya hivyo iwe kwa kutaka au vinginevyo.
Hakuna jambo gumu na hatarishi kama kuombwa ushauri hasa kwenye ndoa ambayo hairekebishiki. Sisi tumewahi kuombwa ushauri.
Katika kutoa ushauri, kuna jambo moja wanandoa wengi huliogopa au kuliepuka, yaani kumwambia mwenye kutaka ushauri aachane na mwenzake.
Wengi huogopa kushiriki dhambi ya kuachanisha wawili walioungana kwa hiari yao. Pia, huchelea madhara yatakayowapata wahusika, watoto, na familia zao.
Hata hivyo, ingawa kushauri wawili waachane kuna ukakasi, kuna kipindi kuachana ni bora kuliko kumalizana.
Tumewahi kuongelea mauaji ya wanandoa wengi wao wakiwa kinamama, na siku hizi, hata watoto kwa upande wa Afrika. Kwa upande wa Amerika, madhara ni kwa yeyote.
Mfano, wapo wanandoa wanaoudhiana ambapo mmoja wao, wengi wakiwa wanaume, huchukua bunduki na kwenda kuua watu wasio na hatia.
Kwa mujibu wa jarida la Bloomberg (2022), nchini Marekani, kati ya mwaka 2014 na 2019, asilimia 60 ya waliotekeleza mauaji ya watu wengi walikuwa ni waathirika wa unyanyasaji wa majumbani, na wengi walikuwa ni wanaume wakati waathirika wakiwa wanawake na watoto. Kuna visa vingi sehemu mbalimbali duniani.
Kama binadamu angekuwa na uwezo wa kuyajua ya kesho, ungeombwa ushauri na watu kama hao hapo juu wanaoua wenzao kutokana na ugomvi wao, ungewashauri nini zaidi ya kuachana?
Kipi bora? Kuogopa kuwatenganisha na watoto nao kuathirika wakati watatengana milele baada ya kusababisha mauaji ya wenzao na wengine wasiohusika au kuwashauri waachane tena kwa amani ili waendelee kuishi wao na wengine ambao matendo na hasira zao vingewaathiri tena vibaya?
Kama mmekutana na kukubali kufunga ndoa kwa hiari, ni kwanini wengi hawapendi au kushindwa kuachana kwa hiari? Tunaishi mara moja.
Hivyo, kuna haja ya kuyaangalia mambo kama yalivyo bila kuchelea lawama. Hivi, utajisikiaje utakapogundua kuwa wale waliokuja kukuomba ushauri ukawashauri waendelee ‘kuvumilia’tu wamemalizana?
Je, hautakuwa umechangia kwenye msiba huu unaoweza kuepukwa kama tutakubali kuupokea uhalisia wa mambo kuwa kuua siyo jibu?
Je, ni kwanini wengi wanaua wenzao tena wasiohusika wala kuwa na hatia? Jibu ni kwamba mifarakano na ugomvi katika ndoa ni chanzo kizuri cha changamoto ya afya ya akili.
Hivyo, mabingwa wa vurugu na udhalilishaji kwenye ndoa, wajue kuwa wanajiletea au kuwaletea wenzao tatizo hili ambalo matokeo yake ni mabaya sana.
Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa udhalilishaji wa majumbani huchangia kwa kiasi kikubwa katika changamoto ya afya ya akili, uraibu, kujiua, msongo wa mawazo, na mengine mengi.
Je, kama tunaoombwa ushauri na kuogopa kushauri wahusika waachane kwa usalama wao na wengine, tungejua ukubwa wa tatizo, tungeendelea kuona kuwa ni dhambi kuwashauri wanandoa waendelee kuvumiliana katika udhalilishaji?
Wadhalilishaji wengi na waathirika wote wana changamoto ya afya ya akili. Japo tunaweza kuwaona ni watu wa kawaida, ndani, wanatukuta na kuficha mengi.
Ni kama volkano iliyolala ikingoja kulipuka. Siku inapolipuka, si rahisi kujua ukubwa wa madhara yake. Hivyo, tunapaswa kuachana na imani za kizamani za kuogopa kuwasaidia wanaotujia wakitaka msaada wa mawazo.
Muhimu, ni kupima kiwango cha uharibifu kilichokwishatokea kwenye ndoa, ndipo iwe rahisi na sahihi kutoa ushauri sahihi.
Japo wanandoa wanaweza kutaka ushauri kwa marafiki, ndugu hasa wazazi, mara nyingi, ndiyo wanaokimbiliwa. Wapo wazazi kwa sababu mbali mbali, huwashauri watoto wao wavumilie.
Hivi, unajisikiaje kuwa binti yenu mliyemshauri aendelee kuvumilia udhalilishaji wa mumewe mliyeagana naye jana kauawa na mumewe? Hivi, kuna dhambi kubwa kama hii?
Wapo wanaowashauri mabinti zao kuendelea kuishi kwenye ndoa hatarishi kwa kuogopa kudaiwa mahari. Hivi mahari ina thamani kuliko uhai wa mtu tena asiye na hatia zaidi ya kupenda?
Tumalize kwa kushauri kuwa unapogundua kuwa uhusiano wa ndugu au rafiki aliyekuja kukuomba ushauri ni hatarishi, usiogope ‘kumpa’ ukweli kuwa kuna wakati kuachana ni bora kuliko kuendelea kuishi kwenye ndoa hatarishi, ambayo matokeo yake yanaweza kuwa vifo na majanga kwa wengine wasiohusika.