Rukwa. Mgombea ubunge wa Sumbawanga mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Aesh Halfan Hilary amesema endapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa atahakikisha changamoto ya pembejeo za kilimo zinatatuliwa na wakulima kuondokana na changamoto hiyo.
Aesh amezungumza hayo leo Septemba 15, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni katika viwanja vya Shule ya Msingi Msua, Manispaa ya Sumbawanga mkoani hapa.
Aesh amesema wakulima wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi ikiwamo ukosefu wa pembejeo za kilimo na kukosa soko la kuuzia mazao yao.
“Mkinipa ridhaa nitahakikisha soko la kimataifa la mazao Kanondo, linakamilika ili wakulima wakauze mazao yao pale, tena kwa bei nzuri,” amesema Aesh.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Siraf Maufi akifungua mkutano huo wa kampeni amewaombea kura madiwani na mgombea ubunge wa jimbo hilo.
Baadhi ya wananchi akiwamo Richard Mtanga amesema endapo ahadi alizozitoa mgombea zitatekelezwa, jamii hiyo itaondokana na changamoto kubwa ya kukosa mbolea ya ruzuku.
“Hatupati mbolea ya ruzuku kwa wakati na wakati mwingine hatupewi taarifa na hatimaye unakuta msimu umekaribia na tunashindwa kulima kilimo cha kisasa kutokana na kukosa pembejeo za kilimo kwa sababu ya uzembe wa viongozi tulionao,” amesema Mtanga.