SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemtangaza mwamuzi Ahmed Arajiga, kuwa mwamuzi wa kati kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii utakaozikutanisha Yanga dhidi ya Simba.
Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, amesema Arajiga atakuwa mwamuzi wa kati katika mchezo huo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ndimbo amesema Arajiga atasaidiwa na Mohammed Mkono, atakayekuwa mwamuzi msaidizi wa kwanza na Kassim Mpanga, atakayekuwa mwamuzi namba msaidizi namba mbili, huku mwamuzi wa nne atakuwa Ramadhan Kayoko.
Rekodi zinaonyesha hii itakuwa ni Dabi ya Kariakoo ya tano kwa mwamuzi huyo kutoka Manyara kuamua mchezo huo.
Yanga ndio wenye bahati na Arajiga, ambapo kwenye mechi nne zilizoamuliwa na mwamuzi huyo, imeshinda tatu na kupoteza moja .
Arajiga anaipokea Dabi hiyo kutoka kwa wamuzi wa Misri, ambao walichezesha mchezo wa mwisho baina ya timu hizo, kwenye kufunga msimu uliopita wa Ligi, ambapo Simba ilichezea kipigo cha mabao 2-0.