Aucho apiga hesabu kali, aitaja Yanga

SINGIDA Black Stars jana ilibeba ubingwa wa kwanza wa Kombe la Kagame kwa kuifunga Al Hilal ya Sudan mabao 2-1, katika mechi ya fainali ya Kombe la Kagame 2025, huku nahodha wa timu hiyo, Khalid Aucho amefichua siri iliyomfanya atue kwa wauza alizeti hao akisisitiza mashabiki wajiandae kupata furaha msimu huu.

Aucho aliyetua Singida baada ya kumaliza mkataba Yanga aliyoitumikia kwa misimu minne, alisema lengo la kujiunga na timu hiyo ni kuhakikisha anasaidiana na wenzake kuipa mataji na kuifikisha mbali katika michuano ya kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aucho alisema Singida ina kikosi kizuri kilichosheheni nyota wengi wenye ubora na uzoefu, hivyo kwa pamoja wakiweka juhudi wana kila sababu ya kutwaa mataji na kuwakilisha vizuri kimataifa.

“Nimekuja Singida kutwaa mataji, siyo rahisi, lakini naamini tukishirikiana vizuri na wenzangu tuliopewa nafasi na kocha tunawez kufikia malengo,” alisema kiungo mkabaji huyo raia wa Uganda aliyeongeza;

“Tuna kila sababu ya kufanya vizuri kwani tuna kikosi kizuri na wachezaji kila mmoja ana malengo ya kufanya vizuri hivyo naamini mambo kama yataenda kama tulivyopanga tunaweza kuwa sehemu ya timu zitakazotoa ushindani kuwania taji na hatimaye kutwaa ndani na kufanya vizuri kimataifa.”

Aucho ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Uganda, The Uganda Cranes akiwa ndani ya timu hiyo ataendelea kuvaa jezi namba nane baada ya kuachiwa na Serge Pokou.

Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Habari wa Singida Black Stars, ili kuzungumzia suala la kitambaa cha unahodha alilithibitishia gazeti hili ni rasmi wamemkabidhi Aucho kitambaa hicho akisaidiana na Kennedy Juma na Morice Chukwu.

“Ndio amepewa kitambaa kama nahodha mkuu wa timu ni kiongozi mzuri kuanzia nidhamu hadi ubora uwanjani hivyo atasaidiana na Juma na Chikwu.”