CAF yaishushia rungu zito Simba, kuikabili Gaborone bila mashabiki

TAARIFA kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), zinasema mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Simba SC itakuwa nyumbani kuikaribisha Gaborone United ya Botswana, itacheza bila mashabiki wake.

Mbali na kucheza bila ya mashabiki mchezo huo wa nyumbani, wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, wamepigwa faini ya Dola 50,000 (Sh123 milioni).

Adhabu hiyo imetokana na tukio la mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita Simba ilipokuwa mwenyeji wa Al Masry, ambapo mashabiki waliingia uwanjani na fataki zilitumika.

Katika mchezo huo uliofanyika Aprili 9, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba ilishinda kwa penalti 4-1 na kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo kufuatia matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2.

Katika adhabu hiyo, CAF imeweka marufuku ya mechi mbili za nyumbani kwa Simba ambapo moja ni dhidi ya Gaborone United hatua ya awali itakayochezwa Septemba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Baada ya hapo, mechi ya pili imewekwa kwa masharti na itatekelezwa endapo tabia hizo zilizokatazwa na CAF zitajirudia msimu huu.

Katika taarifa hiyo, CAF imesema Simba imevunja kifungu cha 82 na 83.2 cha kanuni za nidhamu za shirikisho hilo sambamba na kifungu cha 32, 33 na 35 kuhusu kanuni ya udhibiti wa usalama.

Hii si mara ya kwanza kwa Simba kukumbana na adhabu hiyo kwani msimu uliopita 2024-2025 katika Kombe la Shirikisho Afrika, Januari 19, 2025 timu hiyo iliikabili CS Constantine bila ya mashabiki kufuatia adhabu iliyopewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Adhabu hiyo ilitokana na vurugu katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien uliofanyika Desemba 15, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda kwa mabao 2-1, zilitokea vurugu ambazo zilisababisha viti 256 kuvunjwa.

Mbali na Simba, CAF pia imeifungia Al Ahli Tripoli kucheza bila ya mashabiki mechi ya nyumbani kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Dadjè FC kutoka Benin.

Adhabu hii inatokana na tukio la vurugu kwenye mechi yao ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba SC msimu uliopita wakati hatua ya robo fainali Al Ahli Tripoli iliposhinda 2-0 nyumbani kabla ya kwenda ugenini kufungwa 2-0, na kupoteza kwa penalti 4-1.

Timu nyingine iliyokumbana na adhabu hiyo ni MC Alger inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Adhabu hii imetolewa baada ya vurugu za mashabiki kwenye mchezo wao dhidi ya Orlando Pirates ambapo sasa itacheza mechi ya pili ya mzunguko wa awali dhidi ya Fassell kutoka Liberia bila mashabiki.

Kwa MC Alger, hata mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Algeria msimu huu itachezwa bila mashabiki, kutokana na adhabu tofauti kutoka Shirikisho la Soka la Libya.

Msimu huu, CAF imeendelea kusisitiza kuwa shabiki akivamia uwanja, kutupa vitu, au kutumia fataki, adhabu itaangukia kwa klabu.