Dimwa: Si kila mtua anafaa kuwa Rais, tumpe kura Dk Mwinyi

Unguja. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema urais ni nafasi nyeti ambayo haiwezi kupewa kila mtu, akisisitiza wananchi kumchagua mgombea wa chama hicho, Dk Hussein Mwinyi, kwa kuwa ana maono makubwa ya kuendeleza Zanzibar.

Dk Dimwa ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 15, 2025, katika Uwanja wa Gombani ya Kale Mkoa wa Kusini Pemba wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM huko Pemba baada ya chama hicho kumaliza uzinduzi wake Unguja.

“Urais si jambo la lelemama kwamba apewe kila mmoja. Unastahili kupewa mtu mwenye maono, mitazamo na upeo mpana. Sifa hizi zote anazo Dk Mwinyi na hakuna wa kumfananisha naye,” amesema Dk Dimwa.

Ametaja maeneo sita ya kipaumbele ambayo mgombea huyo ameyapa kipaumbele kwamba ni pamoja na uchumi imara, uongezaji wa ajira, kupunguza umasikini, kuendeleza mapinduzi ya kijani, kuimarisha sekta ya habari na mawasiliano, kuboresha huduma za kijamii pamoja na miundombinu.

Dk Dimwa amebainisha kuwa ndani ya miaka mitano ya uongozi wake, Dk Mwinyi ametekeleza miradi mbalimbali kisiwani humo katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu.

Amesema katika sekta ya elimu pekee huko Pemba, Mwinyi amejenga shule za ghorofa 13 za msingi na sekondari na kuajiri walimu 2,406.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, Mohamed Aboud Mohamed akizungumza katika uzinduzi huo amewataka wananchi kumlipa fadhila Dk Mwinyi kwa kumpigia kura nyingi za ndiyo ifikapo Oktoba 29 huku akisisitiza kuwa ametekeleza mambo makubwa ndani ya kipindi kifupi.

“Wajibu wenu ni kulipa hisani. Neema hii ameileta Mungu. Niamini ndugu zangu Wazanzibari mmeona ubunifu wake, umakini wake na utayari wake wa kuleta maendeleo. Tumchague tena ili aendelee katika awamu ya pili,” amesema Aboud.

Ameongeza kuwa Dk Mwinyi ameimarisha umoja, amani na utulivu bila kuchochea mifarakano, bali amejikita katika kujenga nchi.

“Ndugu zangu, penye shari ugomvi na vita, hata Mungu hashushi neema zake. Tumesikia wapo wanaotaka shari, tuwakatae kwa kura zote na tumpe Dk Mwinyi,” amesema Aboud, akihimiza mshikamano.

Amesisitiza kuwa busara na umahiri wa Mwinyi katika kudumisha amani unapaswa kuungwa mkono ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo.