Dk Nchimbi awatumia ujumbe waliokosa uteuzi ndani ya CCM

Tanga. Mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi, amewataka wanachama wa chama hicho waliokosa fursa za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutulia na kuheshimu uamuzi wa vikao vya chama.

Amejitolea mfano, akisema, mwaka 2005 jina lake lilienguliwa kwenye mbio za kuwania nafasi ya uspika wa Bunge la Tanzania, lakini baadaye ameteuliwa kuwania nafasi kubwa zaidi.

Dk Nchimbi amesema hayo leo, Jumatatu Septemba 15, 2025, katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Wilaya ya Lushoto, eneo la Soni, Jimbo la Bumbuli, Mkoa wa Tanga. Mkutano huo umetumika kueleza mafanikio ya miaka mitano iliyopita katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, kilimo, mifugo na miundombinu, pamoja na kile wanachokwenda kukifanya miaka mitano ijayo 2025-2030.

Mbali na kumwombea kura mgombea urais Samia Suluhu Hassan, wagombea ubunge na udiwani, amezungumzia uteuzi wa kuwania nafasi mbalimbali.


Maelezo hayo yanatokana na mchakato wa ndani wa CCM wa kuwapata wagombea udiwani na wabunge, wakiwamo wa viti maalumu ambao baadhi ya walioongoza kwenye kura za maoni hawakuteuliwa.

Miongoni mwa majimbo hayo ni Bumbuli, ambapo January Makamba aliyeongoza jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 15, licha ya kuongoza kura za maoni, vikao vya juu vya uteuzi vilimteua Ramadhan Singano kuwania ubunge.

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amesema idadi ya wanachama wa CCM hadi sasa imefikia milioni 13.4, na wote hao wana haki ya kuchukua fomu na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

“Kati ya wanachama hao wote, ni mmoja tu anatakiwa kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais, ubunge au udiwani. Sasa chama ndiyo kinaamua nani aende kwenye nafasi hizo na nani asiende.

“Kama mnakumbuka mwaka 2020 baadhi waliongoza katika mchakato wa kura lakini hawakuteuliwa, wakachukuliwa wa chini. Tunapima mapenzi yako kwa nchi na chama chako. Si lazima zamu yako ikawa leo, inaweza kuwa mwakani au siku nyingine zijazo,” amesema na kuongeza;

“Mtu akiachwa leo, siyo maana yake ataachwa tena kesho. Unaweza kuachwa leo na ukateuliwa kesho nafasi nyingine.

“Nitawapa mfano, mwaka 2005 niligombea nafasi ya uspika na Kamati Kuu ikakaa ikaamua nafasi hiyo hainifai. Na leo, imepita miaka 20, nimeteuliwa kuwa mgombea mwenza. Kwa hiyo unaweza kugombea nafasi nyingine lakini ukapata nafasi nyingine tena kubwa. Kila mwana CCM anapaswa kujenga utamaduni wa kuheshimu uamuzi wa chama,” amesema Dk Nchimbi.

Huku akishangiliwa, amesema hata Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, alisema demokrasia bila nidhamu ni fujo. Dk Nchimbi pia amemsihi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Abdilahaman Rajabu, kumhakikishia kuwa kata na majimbo yote yanakwenda CCM.

“Nimezungumza na Katibu Mkuu mstaafu, Luteni Yusuf Makamba, akanihakikishia CCM inashinda majimbo yote ya Tanga. Alitamani aje kwenye mkutano lakini ameshindwa. Na hapo ndipo tunaungana kukijenga chama chetu,” amesema Dk Nchimbi.

Hata hivyo, Dk Nchimbi alimpigia simu Makamba na amewaomba wananchi wa Bumbuli kumchagua Samia, mgombea ubunge wa Bumbuli, Ramadhani Singano na madiwani wote wa chama hicho.

Makamba, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesema anaimani na wagombea wote wa CCM, alipenda kuhudhuria mkutano huo ila tatizo ni changamoto ya afya yake.

Mgombea mwenza huyo amesema kilimo cha umwagiliaji kimeboresha, miradi ya umwagiliaji imeongezeka kutoka 17 hadi 24. Pia, upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 210 hadi 400, na vipimo vya kupima ardhi vimepelekwa Lushoto.


Amesema maofisa ugani wamewezeshwa kwa usafiri na vifaa vya mawasiliano, na kwenye mifugo, chanjo zimetolewa 21,010. Katika maji, miradi zaidi ya Sh5.8 bilioni imekamilika, na kusababisha zaidi ya asilimia 75 ya wakazi wa Lushoto kupata maji.

Amesema barabara za lami zenye urefu wa kilomita 3.5 zimejengwa, na za changarawe 120 zimekarabatiwa. Katika afya, hospitali ya wilaya imejengwa, zahanati 17, kituo cha afya kimoja, na madarasa yamejengwa.

“Tutahakikisha tunajenga zahanati sita, Hospitali ya Wilaya ya Lushoto inaboreshwa kwa kujenga ICU itakayokuwa na uwezo wa kuchukua watu 15 kwa wakati mmoja. Pia kutajengwa jengo la mionzi (X-Ray) na nyumba 20 za watumishi wa hospitali,” ameahidi Dk Nchimbi.

Amesema kwenye barabara zitajengwa barabara zenye urefu wa kilomita 500 za changarawe na kilomita 25 za lami.

“Katika viwanda, hapa Lushoto kutajengwa kiwanda cha kuchakata mkonge na chai, ili mazao yasipotee na kuleta tija katika kilimo,” amesema.

Awali, kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema, “Ukiwa na baba dhaifu, unapata familia dhaifu, na ukiwa na kiongozi dhaifu unakuwa na utawala dhaifu, lakini kwa takwimu za maeneo mbalimbali, zinathibitisha ni kiongozi imara, ndiyo maana tunajivunia mafanikio mbalimbali.”

Akimkaribisha, Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abraham, amesema wamejipanga kupata ushindi wa kutosha katika kata zote zaidi ya 400, na majimbo.