Tanga. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewataka wanachama wa chama hicho waliokosa fursa za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutulia na kuheshimu uamuzi wa vikao vya chama.
Amejitolea mfano yeye mwenyewe akisema, mwaka 2005 jina lake lilienguliwa kwenye mbio za kuwania uspika wa Bunge la Tanzania.
“Lakini nikatulia, miaka 20 baadaye vikao vilevile vimeniteua kuwa mgombea mwenza wa urais, tena nafasi kubwa zaidi.”

Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 15, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Wilaya ya Lushoto, eneo la Soni, Jimbo la Bumbuli, Mkoa wa Tanga.
Mkutano huo umetumika kueleza mafanikio ya miaka mitano iliyopita ya sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, kilimo, mifugo na miundombinu na kile wanachokwenda kukifanya miaka mitano ijayo 2025/2030.
Dk Nchimbi mbali na kumwombea kura mgombea urais, Samia Suluhu Hassan, wagombea ubunge na udiwani, amezungumzia uteuzi wa kuwania nafasi mbalimbali.
Maelezo hayo yanatokana na kile kilichotokea kwenye mchakato wa ndani wa CCM wa kuwapata wagombea udiwani na wabunge wakiwamo wa viti maalumu ambao baadhi ya walioongoza kwenye kura za maoni lakini vikao havikuwateua.

Miongoni mwa majimbo hayo ni Bumbuli, January Makamba aliyeongoza jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 15, licha ya kuongoza kura za maoni, vikao vya juu ya uteuzi vilimteua Ramadhan Singano kuwania ubunge.
Katika mkutano huo amesema, idadi ya wanachama wa CCM hadi sasa imefikia milioni 13.4 na wote hao wana haki ya kuchukua fomu na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.
“Lakini kati ya hao wote ni mmoja tu anatakiwa kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais, ubunge na udiwani. Sasa chama ndiyo kinaamua nani aende kwenye nafasi hizo na nani asiende,” amesema Dk Nchimbi.
Katibu mkuu huyo wa zamani wa CCM amesema:”Kama mnakumbuka mwaka 2020 baadhi waliongoza katika mchakato wa kura lakini hawakuteuliwa, wakachukuliwa wa chini. Tunapima mapenzi yako kwa nchi na chama chako. Si lazima zamu yako ikawa leo inaweza kuwa mwakani au siku zingine zijazo.”
“Mtu akiachwa leo siyo maana yake ataachwa tena kesho. Unaweza kuachwa leo na ukateuliwa kesho nafasi nyingine. Nitawapa mfano mmoja, mwaka 2005 mimi niligombea nafasi ya uspika na Kamati Kuu ikakaa ikaamua nafasi ya uspika hainifai.

“Na leo imepita miaka 20 nimeteuliwa kuwa mgombea mwenza. Kwa hiyo unaweza kugombea nafasi nyingine lakini ukapata nafasi nyingine tena kubwa. Kila mwana CCM anapaswa kujenga utamaduni wa kuheshimu uamuzi wa chama. Lazima tuheshimu demokrasia inayoendana na nidhamu,” amesema Dk Nchimbi.
Huku akishangiliwa, amesema hata Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema dekokrasia bila nidhamu ni fujo na anamshukuru Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Tanga, Abdlahaman Rajabu ambaye amemhakikishia kata na majimbo yote yanakwenda CCM.
“Nimezungumza na Katibu Mkuu mstaafu, Luteni Yusuf Makamba akanihakikishia CCM inashinda majimbo yote ya Tanga. Alitamani aje kwenye mkutano lakini ameshindwa. Na hapo ndipo tunaungana kukijenga chama chetu,” amesema Dk Nchimbi huku wananchi wakishangilia.
Hata hivyo, Dk Nchimbi amempigia simu Makamba na amewaomba wananchi wa Bumbuli kumchagua Samia, mgombea ubunge wa Bumbuli, Ramadhani Singano na madiwani wote wa chama hicho.

Makamba aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema anaimani na wagombea wote wa CCM na alipenda kuhudhuria mkutano huo ila tatizo ni changamoto ya afya yake
Mafanikio, mipango ijayo Mgombea mwenza huyo amesema, kilimo cha umwagiliaji kimeboresha, miradi ya umwagiliaji imeongezeka kutoka 17 hadi 24.
Upatikanaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 210 hadi 400, vipimo vya kupimia ardhi vimepelekwa Lushoto.
Amesema maofisa ugani wamewezeshwa usafiri na vifaa vya mawasiliano, kwenye mifugo chanjo zimetolewa 21,010.
Kwenye maji, miradi ya zaidi ya Sh5.8 bilioni imekamilika na kusababisha zaidi ya asilimia 75 ya wakazi wa Lushoto kupata maji.
Kuhusu barabara, Dk Nchimbi amesema barabara za lami zenye urefu wa kilomita 3.5 zimejengwa, za changarawe 120 zimekarabatiwa.
Katika afya, hospitali ya wilaya imejengwa, zahanati 17, kituo cha afya kimoja na kufanya idadi kuwa vinne na madarasa yamejengwa.
“Tutahakikisha tunajenga zahanati sita, Hospitali ya Wilaya ya Lushoto inaboreshwa kwa kujenga ICU itakayokuwa na uwezo wa kuchukua watu 15 kwa wakati mmoja. Pia kutajengwa jengo la mionzi (X-Ray), nyumba 20 za watumishi wa hospitali zitajengwa,” ameahidi Dk Nchimbi.
Amesema kwenye barabara zitajengwa barabara zenye urefu wa kilomita 500 za changarawe, kilomita 25 za lami. Pia, kutajengwa madaraja na vivuko 25. Shule za msingi tano na sekondari nne zitajengwa, madarasa 400 ya shule za msingi na 300 kwa shule za sekondari yatajengwa. Pia, yatajengwa mabweni 15 na maabara 20.
“Katika viwanda, hapa Lushoto kutajengwa kiwanda cha kuchakata mkonge, chai ili mazao yasipotee na kuleta tija katika kilimo,” amesema.
Awali, kwenye mkutano huo, kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema:”Ukiwa na baba dhaifu, unapata familia dhaifu na ukiwa na kiongozi dhaifu unakuwa na utawala dhaifu, lakini kwa takwimu za maeneo mbalimbali zinathibitisha ni kiongozi imara ndiyo maana tunajivunia mafanikio mbalimbali.”
Akimkaribisha, Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Tanga,
Rajabu Abraham amesema wamejipanga kupata ushindi wa kutosha katika kata zote zaidi ya 400 na majimbo yanakuwa Chama cha Mapinduzi.
Rajabu ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu amesema kazi kubwa imefanyika katika kila sekta, hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi, Oktoba 29, 2025 kumchagua Samia aendelee kubaki madarakani, wabunge na madiwani wote.
Dk Nchimbi atafanya mikutano minne kwenye majimbo mbalimbali mkoani Tanga.
Endelea kufuatilia Mwananchi