KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema katika mechi ya kesho dhidi ya Yanga, hawana presha kwa sababu tayari wana uzoefu na dabi, huku akiamiani benchi la wapinzani wake litakuwa na kazi za ziada kutokana na ugeni wao.
Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii uliopangwa kuchezwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambapo Fadlu itakuwa mara ya pili kucheza mashindano hayo, wakati Kocha wa Yanga, Romain Folz ni mara ya kwanza.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Fadlu amesema: “Kesho ni mechi kubwa lakini malengo yetu ya kwanza ni kuhakikisha tunachukua alama tatu muhimu.
“Yapo mambo ambayo wana Simba walikuwa wanatamani kuona maboresho yake, lakini niwaahidi kwamba kikosi kipo tayari kwa ajili ya mechi hiyo muhimu na kila aina ya makosa madogo madogo ambayo yameonekana tumeyafanyia kazi kwa lengo la kushinda,” alisema Fadlu na kuongeza.
“Jambo kubwa ambalo limeongezeka kwa wachezaji ni jinsi ya kutuliza presha ya mashabiki, lakini pia kucheza kwa utulivu wa hali ya juu wakijua kwamba wanakwenda kucheza na wapinzani wao wakubwa ambao sasa wanaatikiwa kuweka rekodi mpya.
“Rekodi yetu ya kupoteza mbele ya Yanga inatupa motisha ya kujifunza zaidi pale ambapo tumekuwa tukipakosea mara kwa mara ili tusipoteze tena.”
Nahodha wa kikosi hicho, Shomari Kapombe amesema, kwa upande wa wachezaji wako tayari kujitoa kwa asilimia zote kuhakikisha unakuwa mchezo wenye matokeo mazuri, kwani ndio unakwenda kufungua msimu.
“Ukiangalia msimu uliopita Yanga walikuwa na safu nzuri ya ushambuliaji, jambo ambalo lilitugharimu, tutaendelea kupunguza makosa na kuongeza ubora wetu,” amesema Kapombe.
Fadlu anakwenda kuiongoza Simba katika mchezo huo akiwa na kumbukumbu ya kupoteza mwaka jana kwa bao 1-0 hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo. Pia kocha huyo alipoteza mechi zingine mbili za ligi dhidi ya Yanga.