Folz aringia ubora wa mastaa Yanga, aficha jambo hili

KOCHA wa Yanga, Romain Folz, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Simba huku akiringia ubora wa mastaa wa timu hiyo.

Folz amesema, timu hiyo imefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo, huku akikiri kwamba wanakwenda kukutana na timu nzuri yenye wachezaji bora.

Kocha huyo ambaye anayekwenda kucheza dabi ya kwanza tangu atue nchini, amesema anaamini falsafa ya soka anayoitumia na ubora wa wachezaji waliopo Yanga vitakwenda kuipa kikosi hicho matokeo ya ushindi.

“Tupo tayari kwa mchezo wa kesho, tumekuwa kwenye maandalizi makubwa, naweza kusema tupo kwenye eneo zuri ingawa sio kwa kiwango tunachokitaka,” amesema Folz na kuongeza.

“Simba ni timu kubwa, ina wachezaji wazuri kwa hiyo tutakuwa na tahadhari, lakini tutatumia falsafa yetu na ubora wa wachezaji  kupata matokeo.”

Akizungumzia hali ya kikosi chake, Folz amesema, kila mchezaji anaitaka mechi ingawa ana majeruhi, huku akigoma kuwataja.

“Kila mchezaji yuko tayari anapenda kucheza mechi kama hii, kutakuwa na mabadiliko tofauti kulinganisha na ile ya mwisho ya kirafiki, tuna majeruhi ndio lakini siwezi kuwataja.”

Mchezo huo ni wa ufunguzi wa msimu wa 2025-2026 ambapo Yanga inaingia ikiwa na kumbukumbu ya kushinda taji hilo mwaka jana ilipoifunga Azam mabao 4-1.