Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, ametaja mambo matatu makubwa yaliyokuwa kero kwa wananchi wa Kisiwa cha Pemba, lakini amesema Serikali inayoongozwa na Dk Hussein Ali Mwinyi imefanikiwa kuyapatia ufumbuzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akizungumza leo Jumatatu Septemba 15, 2025 kwenye uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) upande wa Pemba uliofanyika Uwanja wa Gombani ya Kale, Mkoa wa Kusini Pemba, Hemed amewaomba wananchi waendelee kuichagua CCM ili huduma hizo ziendelee kuimarishwa.
Amesema changamoto ya kwanza ilikuwa tatizo la wagonjwa waliokuwa wakihitaji kusafisha figo. Kabla ya huduma hiyo kupatikana kisiwani humo, wagonjwa walilazimika kusafiri hadi Unguja kwa gharama kubwa.
“Tatizo hili lilikuwa kubwa sana, wananchi walihangaika kufuata huduma. Mwananchi mmoja alikuwa akitumia takribani Sh600,000 kwa wiki kwa matibabu, lakini sasa huduma ya kusafisha figo inapatikana bure katika Hospitali ya Abdallah Mzee na imeleta faraja kubwa,” amesema Hemed.
Changamoto ya pili amesema ilikuwa tofauti ya bei za vyakula kati ya Pemba na Unguja kutokana na ugumu wa usafirishaji wa bidhaa. Bidhaa zilikuwa zikishushwa Bandari ya Malindi Unguja na kisha kusafirishwa tena Pemba, hali iliyoongeza gharama.
“Mheshimiwa mgombea kilichokuwa kinakera sana ni utofauti wa bei za vyakula. Sasa hivi kuna meli inatia nanga moja kwa moja Bandari ya Mkoani na bei za bidhaa Pemba hazina tofauti na Unguja,” amesema.
Kadhia ya tatu, Hemed amesema ilikuwa upepo mkali uliokuwa ukisababisha ajali na vifo vya wananchi waliokuwa wakisafiri baharini kuelekea Tanga na Kenya kutokana na kukosekana kwa vyombo imara vya usafiri.
“Watu wetu walipotea sana upepo ulipokuwa ukivuma, wengine kuonekana na wengine kutopatikana kabisa. Leo hii kuna vyombo bora vya usafiri vilivyowekwa na sekta binafsi kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Dk Mwinyi, hivyo tatizo hilo limekwisha,” amesema.
Hivyo, amewaomba wananchi wa Pemba kumpa kura nyingi za ndiyo Dk Mwinyi katika uchaguzi wa Oktoba 29, ili amalizie kazi zilizobakia.
“Pahala sahihi pa kupeleka kura zako za urais si pengine bali ni kwa Dk Mwinyi,” amesema Makamu huyo wa Pili wa Rais.