Mbeya. Wagonjwa 230,524 kutoka mikoa mbalimbali nchini wamenufaika na huduma za uchunguzi na upasuaji kupitia kambi maalumu ya madaktari bingwa bobezi wa Mama Samia.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Septemba 15, 2025, na Mratibu kutoka Wizara ya Afya, Dk Ulimbakisye Macdonald, mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, kupokea madaktari bingwa 42 watakaotoa huduma katika halmashauri saba.
Kambi hiyo ilianza Mei 2024 hadi Julai 2025, ikihusisha uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kinamama wakati wa ujauzito, figo, moyo, kisukari na magonjwa ya ndani ya binadamu.
“Huduma hizi zitaanza kutolewa leo Jumatatu, Septemba 15, 2025, hadi Septemba 19 mwaka huu. Lengo ni kuboresha afya za Watanzania kupitia programu ya madaktari bingwa wa Mama Samia,” amesema.
Kuhusu idadi ya wagonjwa wa Mkoa wa Mbeya, Dk Macdonald amesema tangu kuanza kwa kambi hiyo, wagonjwa 2,995 walibainika na matatizo mbalimbali, kati yao 293 walilazwa, 152 wakipewa rufaa na 273 kufanyiwa upasuaji.

Aidha, alisema awamu ya nne ya kambi hii itahusisha madaktari bingwa wa watoto wachanga, wanawake na uzazi, usingizi, magonjwa ya ndani na upasuaji ili kutoa huduma kwa wananchi wenye changamoto.
“Ni wito wetu wananchi wa Mkoa wa Mbeya kujitokeza kwa wingi kufika katika hospitali husika kupata vipimo vya magonjwa mbalimbali na matibabu,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, amewahamasisha wananchi kuhudhuria hospitali za Wilaya kupata huduma, akisema: “Tunaona namna Rais Samia Suluhu Hassan anavyopambania afya za Watanzania, na hii ikiwa awamu ya nne kwa Mkoa wa Mbeya kunufaika.”
Daktari bingwa wa watoto Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH), Dk Anna Magembe, amesema awamu hii Serikali imejipanga kuwafikia wananchi katika halmashauri zote zinazoona changamoto ya kupata huduma.
“Ni mkombozi kwa wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa,” amesema Dk Magembe, akiwahimiza wananchi wa Nyanda za Juu Kusini kutumia fursa hii ya siku tano kupata matibabu ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.
Mkazi wa Kata ya Majengo, Jiji la Mbeya, Jane Fungameza, amesema licha ya Serikali kufikisha huduma hiyo, itabidi pia kuzingatia wananchi wenye kipato duni ili gharama za matibabu zisizowakwamisha.