Butiama. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameiagiza Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kuanzisha jukwaa la wadau wa Bonde la Mto Mara kwa ajili ya usimamizi na uendelevu wa mto huo.
Kanali Mtambi ametoa agizo hilo wilayani Butiama mkoani Mara leo, Septemba 15, 2025, kwenye hitimisho la maadhimisho ya Siku ya Mara.
Amesema kufuatia uwepo wa changamoto nyingi zinazokabili bonde hilo, ipo haja ya kuwa na mipango mikakati itakayoshirikisha wadau mbalimbali ili kuufanya mto huo kuwa salama
Kanali Mtambi amesema miongoni mwa majukumu ya jukwaa hilo yatakuwa ni pamoja na kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za uhifadhi wa bonde hilo na miradi ya maendeleo rafiki kwa mazingira ya Bonde la Mto Mara.
“Pia jukwaa hili litasaidia kuanzisha kampeni ya upandaji miti rafiki ya maji katika eneo lote la Bonde la Mto Mara kupitia Serikali za vijiji, kata, wilaya na mkoa kwa pande zote, yaani Tanzania na Kenya,” amesema.
Kanali Mtambi pia amewataka wananchi wanaozunguka Bonde la Mto Mara kutojihusisha na shughuli zinazohatarisha bioanuai ya mto huo na badala yake wafanye shughuli ambazo ni rafiki kwa uhifadhi.
Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kudhibiti matumizi ya maji yasiyo endelevu katika mto huo kwa ustawi wa jamii nzima.

Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Mara wilayani Butiama mkoani Mara. Picha na Beldina Nyakeke
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Ushirikiano kutoka Shirika la Mpango wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP), Sawiche Wamunza, amesema suala la uhifadhi wa Mto Mara linahitaji ushirikiano kutoka kwa wadau wote.
Amesema ili kuhakikisha Mto Mara unaendelea kuwepo, shirika lake pamoja na mambo mengine limeamua kupanda miti zaidi ya 11,000 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mara.
“Mbali na miti, lakini pia tumeanzisha miradi ya kusaidia akinamama na vijana kwenye masuala ya kilimo ili waweze kufanya kilimo chenye tija kwa mazingira na uchumi wao, kwani tumebaini kuwa masuala ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii nzima ni miongoni mwa sababu ya uwepo wa uharibifu wa mazingira ya mto,” amesema.
Wamunza amesema endapo kundi hilo la vijana na kinamama litawezeshwa kufanya miradi rafiki ya mazingira, wana uwezo wa kuboresha hali zao za kiuchumi kwani fursa zipo za kutosha.
Amesema Mto Mara na Ziwa Victoria ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya ukuaji wa uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki, na kwamba uwepo wa hoteli za kitalii na mgodi wa dhahabu wa Barrick katika Mkoa wa Mara ni fursa muhimu kwa vijana na akinamama kwenye suala zima la kilimo cha mboga mboga na matunda.
“Hii ni kampeni endelevu, na siyo kwa Mto Mara tu, bali kwa ajili ya Ziwa Victoria na mazingira kwa ujumla, itasaidia kuboresha mazingira huku tukiboresha uchumi wa wakazi wa Bonde la Mto Mara,” amesema Wamunza.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dk Masinde Bwire, amesema ikolojia ya Mto Mara ni daraja kubwa na muhimu katika uchumi wa nchi za Afrika Mashariki kupitia sekta ya uchumi.
Dk Bwire amesema moja ya majukumu ya kamisheni yake ni kuhakikisha kunakuwepo na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo ndani ya Bonde la Ziwa Victoria, na rasilimali hizo ni pamoja na Bonde la Mto Mara.
“Tuna kila sababu ya kulinda ikolojia ya Mto Mara kwani ni rasilimali adimu na muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi zetu na watu wake pamoja na viumbe hai, hivyo nitoe wito kwa wadau wote, wakiwemo wananchi, watambue kuwa wana jukumu la kulinda rasilimali hii kwa wivu mkubwa,” amesema.
Akitoa taarifa ya chimbuko la maadhimisho hayo, Mkurugenzi Msaidizi Rasilimali za Maji (Majishirikishi), Robert Sunday, amesema Siku ya Mara inafanyika katikati ya mwezi Septemba kutokana na uwepo wa kilele cha tukio la uhamaji wa wanyama aina ya nyumbu kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania kwenda Maasai Mara nchini Kenya.
Amesema maadhimisho hayo, mbali na kulinda Mto Mara, pia yanasaidia kuimarisha mahusiano na ujirani mwema kati ya nchi hizo za Tanzania na Kenya.
“Maadhimisho haya pia yanasaidia lile lengo la Jumuiya ya Afrika Mashariki la kuhimiza ushirikiano katika suala la uhifadhi wa maji shirikishi,” amesema.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Mbundi, amewataka washiriki wa maadhimisho hayo kutoyachukulia kwa mazoea, bali wazingatie dhima na malengo yake.
“Mto Mara ni uhai wa viumbe hai, binadamu na pia ni nguzo ya uchumi, hivyo shughuli zinazofanyika kwenye eneo hilo lazima ziwe rafiki wa mazingira ya mto,” amesema.
Amesema maadhimisho hayo yanapaswa kutumika katika kuimarisha na kuboresha mshikamano baina ya nchi hizo mbili ili kuhakikisha kunakuwepo na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo