KCMC yaanza kampeni ya siku 90 kukamilisha jengo la matibabu ya moyo

Moshi. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, imezindua kampeni ya siku 90 za kuchangia fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la matibabu na upasuaji wa moyo, huku Sh3.1 bilioni zinahitajika kukamilisha mradi huo.

Hatua hiyo inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wanaolazimika kusafirishwa hadi Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam kwa matibabu.

Ujenzi wa jengo hilo ambao kwa sasa umefikia asilimia 40, utagharimu Sh12.2 bilioni hadi kukamilika kwake na tayari washirika wa kimataifa wamechangia Sh9.1 bilioni, hivyo kwa sasa zinahitajika Sh3.1 bilioni.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema jengo hilo litakapokamilika litaweza kulaza wagonjwa 100 kwa wakati mmoja na kuhudumia zaidi ya wagonjwa 14,000 kwa mwaka, likiwa na huduma kamili za matibabu na upasuaji wa moyo kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini na nchi nzima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Profesa Gileard Masenga, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 90 za kuchangia ujenzi wa jengo la matibabu ya Moyo.



Amesema kwa sasa wagonjwa wengi wa moyo wanalazimika kusafiri hadi Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam, jambo linalosababisha msongamano na gharama kubwa kwa familia.

“Mradi huu utasaidia kugundua mapema magonjwa ya moyo, kupunguza msongamano JKCI na kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania,” amesema Profesa Masenga.

Aidha, ametoa wito kwa wadau mbalimbali zikiwamo kampuni za biashara, mashirika ya dini, taasisi za kiraia na wananchi wote kushiriki kuchangia ujenzi huo akisisitiza kuwa, kila shilingi itakayochangwa ni jiwe muhimu katika ujenzi wa jengo hilo.

Akizindua kampeni hiyo  Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amesema magonjwa ya moyo yameendelea kuongezeka hadi kwa watoto na kuomba wataalamu kufanya tafiti kwa kina ili kubaini visababishi hasa vya maradhi hayo.

Ametumia pia nafasi hiyo kutoa rai kwa Watanzania wote kujitokeza kuchangia ujenzi wa jengo hilo, ili liweze kukamilika kwa wakati na kusaidia wagonjwa ambao kwa sasa hulazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma za matibabu ya moyo.

“Jambo la afya ni muhimu sana kwa binadamu, yapo magonjwa mengi lakini ugonjwa wa moyo ni mkubwa. Nitoe rai kwa Watanzania tuungane na KCMC ili kuhakikisha ujenzi wa jengo hili unakamilika ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya moyo hapa Kilimanjaro,” amesema Babu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanlink Healthcare Foundation, Dk Siraj Mtulia amesema taasisi hiyo imejikita katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa Watanzania kupitia elimu, tafiti, ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali pamoja na kuendeleza huduma za kibingwa, hususan kwa wananchi wa kipato cha chini.

Amesema vituo vya matibabu ya moyo vyenye hadhi ya JKCI, kulingana na idadi ya watu Tanzania, vinahitajika 40 lakini kwa sasa kiko kimoja na kikikamilika cha KCMC kitakuwa kituo cha pili.

Aidha, amewataka Watanzania kushirikiana kwa dhati kupitia kampeni hiyo kwa kuchangia fedha, rasilimali au kuwa mabalozi wa ujumbe huo, akisisitiza kauli mbiu ya kampeni: “Kila pigo la moyo linahesabiwa na kila maisha ya Mtanzania yanathaminiwa.”

Jengo la matibabu na upasuaji wa moyo linalojengwa katika Hospitali ya KCMC



Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto katika Hospitali ya KCMC, Dk Ronald Mbwasi, amesema idadi kubwa ya watoto wenye matatizo ya moyo huzaliwa nayo.

“Kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa hai, 17 huwa na matatizo ya moyo. Katika Kanda ya Kaskazini pekee, makisio yanaonesha zaidi ya watoto 4,000 huzaliwa kila mwaka na changamoto ya moyo lakini wengi hutambuliwa wakiwa wamechelewa, jambo linalopunguza nafasi ya kuokoa maisha yao,” amesema.