Mahakama itakavyomua hatima kesi ya uhaini wa Lissu leo

‎Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la usikilizwaji wa kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ambao utaamua hatima ya kesi hiyo.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa leo Jumatatu, Septemba 15, 2025 na jopo la majaji watatu waliopangwa kusikiliza kesi hiyo, Dunstan 6 (Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Iringa na kiongozi wa jopo) James Karayemaha, kutoka Mahakama Kuu Songea na Ferdinand Kiwonde, kutoka Mahakama Kuu Bukoba.

Katika uamuzi huo, mahakama inapaswa kuamua ama kwa kuzikubali au kuzikataa hoja zote au baadhi za pingamizi hilo la Lissu, alizozibainisha akidai kuwa ni kasoro za kisheria zinazoifanya kesi hiyo kuwa batili.

Hoja zitakazoamua hatima ya kesi hiyo

Kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali (PH), yaani mshtakiwa kusomewa na kujibu shtaka na kisha kusomewa maelezo ya awali ya kesi, Septemba 8, 2025.

Hata hivyo, Lissu aliibua pingamizi la awali akiiomba mahakama iifute kesi hiyo, akitoa sababu mbili, mosi kuwa hati ya mashtaka ni batili na mbili, kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza.

Hivyo, mahakama ilielekeza kusikiliza na kuamua kwanza sababu ya mamlaka ya mahakama kwa kuwa uamuzi unaweza kuwa kwa kesi hiyo. Katika sababu hiyo amebainisha hoja mbili.

Ubatili wa mwenendo kabidhi

Mwenendo kabidhi (committal proceedings), ni mwenendo wa uhamishaji kesi kutoka mahakama ya chini na kuikabidhi Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kuisikiliza.

Anadai mwenendo kabidhi huo, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu ni batili kwani uliendeshwa bila kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023, vifungu vya 263, 264, 265 na 266, vinavyohusiana na mwenendo kabidhi.

Ukiukwaji huo wa sheria alioudai Lissu ni pamoja na alidai kuwa kwanza, mahakama kumkatalia kuorodhesha majina ya mashahidi wake aliowataja, Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Pia, kesi kuahirishwa mara kadhaa bila kutoa sababu, kutokupewa kumbukumbu kamili za mwenendo wa kesi hiyo katika hatua ya ukabidhi, hasa badhi ya nyaraka ambatanisho zinazohusiana na kesi, kuzuia mwenendo kabidhi kurushwa mubashara mitandaoni.

‎‎Mamlaka ya mahakama ya ukabidhi

‎‎Lissu alidai kuwa Mahakama hiyo (Mahakama Kuu) haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa kwanza imepelekwa hapo kutoka katika Mahakama ya Ukabidhi ambayo haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza katika hatua ya ukabidhi.

Alifafanua kuwa Mahakama ya Kisutu iliyoendesha mwenendo kabidhi haikuwa na mamlaka hayo kisheria kwani mwenendo huo ulipaswa kuendeshwa na mahakama ya mahali alikomatiwa yaani Mbinga mkoani Ruvuma, kama sheria inavyoelekeza na si kosa linakodaiwa kutendeka.

Jamhuri kupitia jopo la mawakili wa Serikali linaloongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga lilijibu madai yake hayo ilidai kuwa hayana mashiko.‎

‎‎Kuhusu mashahidi aliowataja, Wakili Katuga alidai kuwa Rais ana kinga ya kuwa shahidi kwa mujibu wa Sheria ya Masuala ya Rais, kifungu cha 10, na kwamba ndio maana Mahakama ya Kisutu haikuwaorodhesha.

Alidai kuwa mahakama hiyo ilimwelekeza Lissu kuwa atawataja mashahidi wake Mahakama Kuu na kwamba Lissu hakutaja mashahidi wake wengine wasio na kinga.

‎Kuhusu kutokahtakiwa alikokamatiwa Mbinga Ruvuma, Wakili Katuga alidai kuwa mtu amshtakiwa katika Mahakama ya mahali alikofanyia kosa na kwamba japo alikamatiwia Mbinga lakini kosa alikofanyia Dar es Salaam.

Katika hoja mbadala aliiomba Mahakama Kuu kama itakubaliana na hoja za Lissu kuwa kulikuwa na kasoro katika mwenendo kabidhi, basi nafuu yake ni kuamuru kesi hiyo irejeshwe Kisutu isikilizwe upya katika hatua hiyo.

Lissu alipinga hoja hiyo akidai kuwa kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuendesha mwenendo kabidhi basi Mahakama Kuu haina mamlaka kuamuru kesi hiyo irudi Kisutu, wala Mbinga kwani huko hawana mashtaka dhidi yake bali imwachilie huru.

Mahakama katika uamuzi wake kama itakubaliana na hoja za Jamhuri na kutupilia mbali hoja za pingamizi la Lissu basi sasa itaendelea na usikilizaji wa sababu ya kwanza ya pingamizi la Lissu kuhusu ubatili wa hati ya mashtaka.

Uamuzi wa hoja hiyo ndio utakaotoa hatima ya kesi hiyo kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo, kufutwa au kurejeshwa Mahakama ya Kisutu.

Hata hivyo kama Mahakama itakubaliana na hoja za Lissu basi itaamua ama kuifuta kesi hiyo na kumwachilia huru Lissu au itaamuru irejeshwe Kisutu kurekebisha kasoro hizo, akashtakiwe Mbinga.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

‎Alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka hilo Aprili 10, 2025, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, maarufu kama Mahakama ya Kisutu, ilikofunguliwa kwa ajili ya maandalizi ya awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, yenye mamlaka ya kuisikiliza.

‎‎Agosti 18, 2025, baada ya taratibu za awali kukamilika, kesi hiyo ilihamishiwa rasmi Mahakama Kuu kwa usikilizwaji.