Dar es Salaam. Wadau wa demokrasia nchini wametaja hatua zinazofaa kuchukuliwa kuimarisha mifumo ya demokrasia na kupendekeza mambo 7 muhimu ya kufanyiwa kazi likiwamo suala la kuandikwa kwa Katiba mpya.
Kauli za wadau hao zimetolewa leo Jumatatu Septemba 15, 2025 katika maadhimisho ya siku ya demokrasia duniani yaliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadam (LHRC) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam yakihusisha wadau kutoka taasisi za kiraia.
Miongoni mwa mambo hayo saba ni pamoja na kuandikwa kwa Katiba mpya, kuruhusiwa kwa mgombea binafsi au huru, kuwapo na mabadiliko ya sheria kandamizi, malezi bora ya familia, mitandao ya kijamii na uhuru wa habari.
Suala la Katiba mpya itakayozaa Tume Huru ya Uchaguzi kimekuwa kilio cha muda mrefu cha wadau wa demokrasia nchini kutokana na Katiba ya sasa kutajwa kuwa na ibara nyingi zilizotungwa chini ya mfumo mmoja wa chama cha siasa.
Wadau hao wametaja haja ya mabadiliko ya katiba na mageuzi ya kisiasa, ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na demokrasia shirikishi, yenye uwajibikaji na inayowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayowagusa.
Katiba na changamoto za sasa
Mchambuzi wa masuala ya siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Deus Kibamba ameeleza kuwa Tanzania haiwezi kupiga hatua ikiwa itaendelea kusimama na katiba ya mwaka 1977 iliyoandikwa kwa mfumo wa chama kimoja.
Akifafanua hoja hiyo, amesema vifungu mbalimbali katika ibara zaidi ya nane za katiba hiyo zimeweka vikwazo vya kidemokrasia vikiwemo vinavyokataza wagombea binafsi, jambo linaloenda kinyume na misingi ya demokrasia ya kisasa.
“Katiba yetu imewanyima wananchi haki ya kugombea nafasi za uongozi bila kupitia vyama vya siasa, huu si msingi wa kidemokrasia, hivyo hatuna budi kuandika Katiba mpya,” amesema Kibamba katika maadhimisho hayo.
Kibamba amepongeza wagombea wa urais wanaotoa ahadi yakusimamia mageuzi ya Katiba nchini akidai hiyo itakuwa hatua muhimu kufikia demokrasia ya kweli.
“Nawapongeza wagombea wanaothubutu kuahidi kwamba wakipewa ridhaa watahuisha mchakato wa katiba mpya, hili ni jambo la dharura la kitaifa,”
Pia, amekumbushia kauli ya Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mwaka 1990 aliwahi kusisitiza wakati nchi ikijiandaa kuingia vyama vingi kuwa kabla ya kuruhusu mfumo huo, ilikuwa lazima kwanza kuandika katiba mpya na mifumo ya sheria.
Pia amenukuu Tume ya Jaji Francis Nyalali ambayo ilipendekeza sheria 40 zilizopo ndani ya katiba ya sasa ya Tanzania ya 1977, zibadilishwe ili kuweka msingi wa vyama vingi, lakini utekelezaji wake umesuasua kwa miongo minne sasa.
Viti maalum na usawa wa kijinsia
Suala la usawa wa kijinsia nalo limeibuka katika mjadala wa hatua za kuimarisha demokrasia nchini ambapo wadau wamesema licha ya hatua zilizopigwa, mfumo bado ni wa upendeleo na hauko sawa wakitaja maboresho yanayohitajika.
“Sheria ya usawa wa kijinsia ya 1998 ilipatikana baada ya mapambano makubwa ya wanawake, lakini bado hatujafikia usawa wa kweli kwani mapambano yametegemea upande mmoja, wa wanawake pekee,”amesema Kibamba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji Mstaafu wa LHRC, Hellen Kijo Bisimba, ametaja mfumo wa viti maalum kama kikwazo katika kufikia usawa huo akidai unawaondoa wanawake katika kusimama kwenye nafasi za kugombea majimbo.
“Hivi viti vilianzishwa kupitia Mkutano wa Beijing kama daraja la muda kuwawezesha wanawake kupata uzoefu ili kuandaa mazingira ya kuwaingiza kwenye nafasi za maamzi lakini sasa vimegeuka kuwa nvya kudumu,” amesema.
“Badala ya wanawake kushiriki moja kwa moja kwenye majimbo ya uchaguzi, wamesukumwa kwenye viti maalum zaidi, mfumo huu unapaswa kutazamwa upya kwa sababu unazalisha utegemezi badala ya usawa wa kweli,” amesisitiza.
Mwanazuoni Dk Ananilea Nkya asema kuwa Tanzania iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi ikiwa na Katiba ya muundo wa chama kimoja cha siasa hali anayodai imefanya Taifa kuwa na siasa chafu na kufifisha ustawi wa demokrasia nchini.
“Tanzania iliingia mfumo wa vyama vingi ikiwa na katiba ya mifumo wa chama kimoja na haijawahi kubadilishwa, hili ndilo chimbuko la matatizo tunayoyaona kwenye mifumo yetu ya kisiasa,” amesema Dk Ananilea na kuongeza kuwa:-
“Tumeshuhudia siasa za kibabe, siasa za kununua wapiga kura, siasa za uchawa na siasa za wenye fedha. Hii imerudisha nyuma ushiriki wa makundi mbalimbali, si wanawake pekee bali pia wanaume wasio na mtaji wa kifedha kushiriki,” amesema.
Ameongeza kuwa vyama vya siasa haviwezi kuunda mifumo ya usawa wa kijinsia bila kuwa na katiba mpya inayoweka misingi hiyo kwa uwazi akisema:-
“Uongozi umegeuka kuwa mali ya watu wachache, ni lazima tufanye mabadiliko ya katiba ili kurejesha uhalali wa mfumo wetu wa demokrasia ya vyama vingi,” amesema.
Kwa upande wake, Mhadhiri na Mchambuzi wa siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Consolata Sulley, akichangia mada katika maadhimisho hayo ameonya kuhusu dhana maarufu kuwa “adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe” akisema ni nadharia inayodhoofisha jitihada za kupigania usawa katika jamii.
“Wanawake wengi wenye uwezo hawajapata nafasi kwa sababu mifumo iliyopo inawabana, ukiachilia mbali ubovu wa katiba, mila kandamizi na dhana potofu kwa baadhi ya wanawake zinatengeneza mazingira magumu ya ushiriki wa wanawake,” amesema.
Dk Consolata amesema jamii inapaswa kubadili mtazamo juu ya wanawake na wanaume, iondoke kwenye dhana hiyo na kuwa na Taifa la utu na haki zaidi ya kuangalia jinsia na kuachana na mifumo dume au mifumo jike.
Kuhusu maendeleo ya teknolojia na udhalilishaji wa kijinsia, Helen Kijo Bisimba, ameitaka jamii kutambua matumizi sahihi ya teknolojia hiyo na kuepuka kudhalilisha watu au kujidhalilisha wahusika wenyewe katika demokrasia.
“Tatizo la udhalilishaji wa kijinsia hasa mitandaoni linapaswa kushughulikiwa kupitia utoaji wa elimu inayoendana na zama za kidijitali tulizonazo kwani wapo wanaojidhalilisha na wanaoonesha kufurahia kudhalilishwa kwao mitandaoni”
Amesisitiza kuwa hii ni changamoto ya elimu ya kujitambua ambayo inapaswa kushughulikiwa si kwa misingi ya jinsia pekee, bali kwa kuzingatia utu wa kila mtu.
Kongamano hilo limehitimishwa kwa maazimio saba makubwa huku katika pendekezo mojawapo, wadau wamesisitiza kuwa Tanzania imerudi nyuma katika demokrasia na hivyo kuna haja ya mabadiliko ya Katiba mara moja.
Wamependekeza Katiba mpya iandikwe upya ili kuweka msingi wa vyama vingi na kuondoa pengo la katiba ya chama kimoja na kupendekeza kuruhusiwa wagombea binafsi ili kuongeza wigo wa ushiriki wa wananchi katika nafasi za uongozi.
Pia wametaka sheria zinazominya uhuru wa kujieleza, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, zifanyiwe marekebisho ili kulinda haki za msingi za raia kutoa maoni na kupata taarifa bila vikwazo vya kisheria.
Mbali na mapendekezo hayo, wametilia mkazo umuhimu wa malezi ya familia na elimu kwa jamii katika kupunguza dhana potofu kuhusu usawa wa kijinsia, wakisema mfumo wa viti maalum ulipaswa uwe wa muda na si wakudumu.
Halikadhalika, kongamano limesisitiza maadili katika matumizi ya mitandao ya kijamii, huku likikemea tabia ya kuchafua watu mtandaoni na siasa za uchawa zinazopotosha dhana ya uongozi bora na viongozi kuwajibika.
Katika hatua nyingine, kongamano hilo limetoa wito kwa mamlaka zinazohusika kulinda na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari kama msingi muhimu wa kulinda demokrasia nchini kuhakikisha uhuru huo hauminywa.
Akizungumzia hilo, Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Fugence Masawe ameonya kuwa kufungiwa kwa vyombo vya habari na majukwaa ya mijadala mitandaoni, akitaja mtandao wa Jamii Forums na mtandao wa X (Twitter), ni pigo kubwa kwa demokrasia.
“Tunajenga taswira mbaya kimataifa pale uhuru wa vyombo vya habari unapominywa, kufungiwa kwa Jamii Forums na Kufungwa kwa Mtandao wa Twita nchini hayaleti sura nzuri kidemokrasia,” amesisitiza.
Aidha, ametoa wito kwa wadau kukaa mezani, kurekebishe kasoro zilizopo ili kupata misingi bora na siasa safi kwa ustawi wa jamii nchini.