Mbongo amkuna kocha Rayon Sports

KOCHA wa Rayon Sports, Fleury Rudasingwa amemtaja kipa wa Kitanzania, Husna Mpaja, kama moja ya vipaji ambavyo wamebahatika kuwa navyo kwenye kikosi hicho.

Mpaja alisajiliwa na mabingwa hao wa Ligi ya Wanawake Rwanda akitokea Geita Queens ya mkoani Geita ambako alicheza na kuonyesha kiwango bora.

Aliongeza kuwa bado hajampa nafasi kutokana na ugeni wa michuano kama CECAFA, akiamini anaweza kuwa bora zaidi kwani ni golikipa wa kisasa.

“Tunafurahi kumpata Husna kwenye kikosi chetu. Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa uwanjani, hasa katika eneo la magolikipa. Tunaamini atatupa nguvu mpya na kuongeza ushindani ndani ya timu,” alisema kocha huyo na kuongeza:

“Kwa sasa tuko kwenye michuano ya CECAFA, na usajili kama huu unatupa matumaini makubwa kuelekea msimu ujao wa ligi. Ingawa sijaanza kumtumia, lakini mazoezini anaonyesha kitu kikubwa.” Kwenye michuano ya CECAFA, Rayon Sports ndiyo mara ya kwanza kushiriki mashindano hayo, ikifika hatua ya nusu fainali.