Geita. Mgombea ubunge wa Jimbo la Geita Mjini, Chacha Wambura amesema endapo atachaguliwa kuongoza jimbo hilo kwa kipindi cha 2025/30 kipaumbele chake cha kwanza ni kuboresha sekta ya elimu, maji, afya na miundombinu ya barabara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Nyaseke, Kata ya Bulela leo Septemba 15, 2025, mgombea huyo amesema kipaumbele cha kwanza ni kuongeza vyumba vya madarasa, mabweni, nyumba za walimu na kujenga shule mpya ili kukabiliana na changamoto za elimu katika maeneo mbalimbali ikiwamo Shule ya Msingi Gamash.
Katika sekta ya afya, ameahidi kujenga zahanati na vituo vya afya pamoja na kuhakikisha kituo cha afya Bulela kuna gari la wagonjwa kuwasaidia wagonjwa watakaohitaji huduma kwenye hospitali kubwa.

Kuhusu changamoto ya maji, amesema mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria utafikisha huduma hiyo kwa vijiji vya Nyaseke, Shiloleli na Bulela, lakini kabla ya utekelezaji wake kamili, visima vitachimbwa na pampu kufungwa ili wananchi waache kunywa maji ya kwenye madimbwi.
Aidha, ameahidi kukarabati miundombinu ya barabara zikiwamo kilomita 41 zilizopo kwenye ilani ya CCM zitakazojengwa kiwango cha lami.
Amesema katika kipindi chake atafuatilia ujenzi wa Barabara ya Geita – Kakola ambayo ni kilio cha muda mrefu ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami na kuondoa adha ya wananchi kusafiri kupitia Bukombe kwenda Kahama.
Vilevile, amesema Serikali inajipanga kujenga ‘shopping mall kubwa’ mjini Geita, sanjari na kubuni miradi ya kiuchumi ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuwawezesha wanawake kupata mikopo yenye tija kupitia elimu ya biashara na mikopo.
“Tutakaa na mgodi kuona namna gani vijana wetu watapata ajira. Kila mama atakayehitaji mkopo atapewa mafunzo na kuandikiwa andiko ili apate mkopo na

kuufanyia kazi kwa tija,” amesema.
Mgombea udiwani Kata ya Mtakuja, Costantine Morand amewataka wananchi kuwapa kura wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais ili kutekeleza ilani ya chama hicho kwa ufanisi.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, wameeleza changamoto kubwa kuwa ni ukosefu wa maji, ajira na ubovu wa barabara.
“Akifanikiwa kumtua mama ndoo kichwani atakuwa ameondoa changamoto kubwa ya muda mrefu,” amesema Cosmas, mkazi wa Nyaseke.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita, Barnabas Mapande amesema chama hicho kimefanikisha utekelezaji wa ahadi nyingi za mwaka 2020 ukiwamo ujenzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na vituo vipya vitano vya afya.