Mpina akatwa tena kinyang’anyiro cha urais Tanzania

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeengua rasmi jina la mgombea wa urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina katika orodha ya wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Hatua hiyo imekuja baada ya INEC kukubali pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari dhidi ya uteuzi wa Mpina. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na INEC leo Jumatatu, Septemba 15, 2025 imeeleza kuwa tume iliketi leo na kufanya uamuzi juu ya jumla ya mapingamizi manne yaliyowasilishwa.

“Katika maamuzi hayo, mapingamizi matatu yaliyowasilishwa na wagombea wengine wa urais akiwamo Almas Hassan Kisabya wa NRA, Kunje Ngombale Mwiru wa AAFP na Mpina mwenyewe dhidi ya Samia Suluhu Hassan wa CCM, yamekataliwa. Hata hivyo, pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mpina limekubaliwa na kusababisha jina lake kufutwa kwenye orodha ya wagombea wa urais,” imeeleza taarifa hiyo.

Endelea kufuatilia Mwananchi.