Mpina aondolewa mbio za urais, akwaa kwa Samia

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imemuondoa mgombea urais kupitia Chama cha ACT – Wazalendo, Luhaga Mpina kwenye mbio za urais, baada ya pingamizi lililowekwa dhidi yake na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari kukubalika.

Wakati huo huo, pingamizi aliloweka Mpina dhidi ya mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, limetupwa.

Taarifa hiyo ya pingamizi za uteuzi wa wagombea wa kiti cha urais imetolewa leo Jumatatu Septemba 15, 2025 na INEC.

Kulingana na taarifa hiyo, Tume imekubali pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, dhidi ya uteuzi wa Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT- Wazalendo.

“Jina la Luhaga Mpina, mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo limeondolewa kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Ikifafanua zaidi, INEC imeeleza kuwa ilipokea mapingamizi matatu dhidi ya uteuzi wa  Mpina na Septemba 14, 2025, INEC ilipokea pingamizi moja dhidi ya uteuzi wa Samia Suluhu Hassan, mgombea wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi.

“Tume katika kikao chake kilichofanyika tarehe Septemba15, 2025 imefanya uamuzi wa mapingamizi hayo manne yaliyowasilishwa mbele yake na mapingamizi matatu yamekataliwa na moja limekubaliwa,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya INEC imeeleza pingamizi lililotupiliwa mbali Mosi ni lile lililowekwa na  mgombea wa kiti cha urais kupitia Chama cha NRA Almas Kisabya dhidi ya Mpina.

Pili, ni pingamizi lililowekwa na mgombea urais kupitia chama cha AAFP, Kunje Ngombale Mwiru dhidi ya Mpina.

Pingamizi la tatu ambalo tume hiyo imetupilia mbali ni pingamizi lililowekwa na Mpina dhidi ya uteuzi wa Samia Suluhu Hassan mgombea urais kupitia CCM.

“Tume imekubali pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari dhidi ya uteuzi wa Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo.

Hivyo, jina la Mpina, mgombea wa kiti cha Rai kupitia Chama cha ACT-Wazalendo limeondolewa kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025,” amesema.