Mpina giza nene sakata la urais Tanzania

Dar es Salaam. Ni rasmi sasa ndoto ama harakati za Luhaga Mpina kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, zimefikia tamati.

Hatua hiyo inatokana na Mpina, aliyewahi kuwa Mbunge wa Kisesa kwa miaka 20 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kukihama chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo.

Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano, alijiengua CCM baada ya jina lake kukatwa kwenye hatua za awali alipochukua fomu ya ubunge kutetea nafasi yake Kisesa.

Hata hivyo, aliibukia ACT-Wazalendo ambako alichukua fomu ya kuwania urais na kupitishwa wakati ambao chama hicho tayari kilikuwa kimteue Kiongozi wake, Dorothy Semu kupeperusha bendera ya chama hicho.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa, Semu aliombwa kujiondoa ili kumwachia Mpina nafasi hiyo. Hata hivyo, tangu Mpina kuingia na kupewa nafasi hiyo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo kwa kura za kishindo, filamu zikaanza kuhusu uteuzi wake.

Kulingana na Katiba ya Tanzania ibara 74(11) ikisomwa pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani  Na 1, 2024 pamoja na kanuni za uchaguzi 2025 katika hatua za mapingamizi, uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) utakuwa wa mwisho na ukishatoka hauwezi kuhojiwa na Mahakama yoyote nchini.

Kutokana na sheria hiyo, Mpina hana tena nafasi ya kugombea urais baada ya kuwekewa pingamizi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari kwa kile kilichoelezwa kuwa amekosa sifa stahiki za kugombea kiti cha urais.

“Tume imekubali pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari dhidi ya uteuzi wa Mpina kuwa mgombea wa kiti cha Rais kupitia chama cha ACT-Wazalendo.

“Hivyo, jina la Mpina, mgombea wa kiti cha Rais kupitia chama cha ACT-Wazalendo limeondolewa kwenye orodha ya wagombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025,” imeeleza taarifa ya INEC kwa umma.

Wakati tume ikikubali pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilikataa na kutupilia mbali mapingamizi mawili yaliyowekwa na Almas Hassan Kisabya, mgombea urais kupitia chama cha NRA na Kunje Ngomale Mwiru, mgombea urais kupitia chama cha AAFP dhidi ya uteuzi wa Mpina.

Pia, tume imekataa pingamizi lililowekwa na Mpina dhidi ya Samia Suluhu Hassan, mgombea urais kupitia CCM.

Mpina mwenyewe alipoulizwa kuhusu uamuzi wa INEC kumuengua, amesema hana cha kujibu kwa kuwa taarifa hizo ni za mitandaoni na kwamba, hajafahamu aliyetoa taarifa hiyo.

“No comments kwa sasa, hizo ni taarifa za mtandaoni, ni nyaraka ambayo na mimi nimeiona kwenye mitandao na sifahamu ni ya nani,” amesema Mpina alipoulizwa na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kutoka Mahakama Kuu kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Hata hivyo, uongozi wa ACT-Wazalendo umepinga uamuzi huo wa INEC na kutangaza kutokubaliana nao, huku wakilalamikia kuminywa kwa demokrasia kwenye suala la uteuzi wa Mpina.

Itakumbukwa kuwa Agosti 14, 2025 aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ACT- Wazalendo, Monalisa Ndala aliandika barua kwa chama hicho kupinga uteuzi wa Mpina kuwania urais kupitia chama hicho akidai ulikiuka kifungu cha 16(1) (4)I ya taratibu za uendeshaji wa chama huku nakala akiwasilisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Msajili aliitisha kikao kikihusisha uongozi wa ACT-Wazalendo ukiongozwa na Katibu mkuu wake, Ado Shaibu na Monalisa akiwa na mawakili wake, ambapo baada ya Ofisi ya Msajili iliitarifu INEC kuwa, Mpina hastahili kuteuliwa kwa kuwa hana sifa. Kupitia hoja hiyo INEC ilisitisha kupokea fomu za uteuzi wa Mpina hivyo, ACT kukimbilia mahakamani kutafuta haki.

Septemba 11, 2025 Mahakama Kuu Masijala Kuu-Dodoma, ilimrejesha Mpina kwenye kinyang’anyiro cha urais baada ya kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba, Evaristo Longopa na John Kahyoza.

Katika hukumu yao, majaji walisema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni huru na haikupaswa kusikiliza maelekezo ya mtu au taasisi yoyote, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Pia, Mahakama hiyo iliiamuru INEC impe fursa Mpina kuwasilisha fomu zake na mchakato uendelee ulipoishia, jambo ambalo lilifanyika.

Hata hivyo, pingamizi la Johari limekwenda kuzima ndoto za Mpina na tayari INEC imetangaza kumuengua rasmi, huku wachambuzi wa masuala ya siasa wakiwa na mitazamo tofauti kuhusiana na sakata zima la uteuzi wake.

Wakili wa kujitegemea, Maduhu William amesema kwa kuzingatia Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2024, ndoto ama hatima ya Mpina kuhusu kugombea urais imefikia mwisho.

“Mpina nafasi yake haipo tena, ingawa uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa ilikuwa bado, hawakwenda kupinga wana nafasi ya kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania kuomba ifanye mapitio kama msajili alikuwa sahihi au hakuwa sahihi,” amesema Maduhu.

Kwa upande wake, Profesa Abel Kinyondo amesema kuna mwanasiasa huyo huenda hana mtu wa kumshauri kuhusu masuala ya kisiasa yalivyo.

“Alikwenda kugombea ubunge, maana yake alitaka kuendelea kuwa mbunge baada ya kuenguliwa CCM, alihamia ACT – Wazalendo, mara akateuliwa kuwa mgombea urais, unaona kabisa ni mtu ambaye hajashauriwa vizuri. Ni katika muda gani aliona agombee ubunge au urais,” amehoji.

Amesema kuwa iwapo Mpina alikuwa na ndoto za kuwania urais angeweza kuchukua fomu akiwa ndani ya CCM ama angetangaza nia hata kama angekosa nafasi hiyo, lakini kuhamia kwake ACT – Wazalendo kulijenga mazingira tatanishi.

“Mpina akiwa CCM alichukua fomu ya ubunge, alipokwenda ACT –Wazalendo akachukua fomu ya kugombea urais, hili ni tatizo tayari. Alikuwa na ndoto ya kuendelea kuwa mbunge ama Urais? Jambo la pili alitakiwa kujiuliza swali dogo tu umehamia kwenye chama kipya, hapo hapo unapewa fomu ya kugombea urais, hilo umeliona wapi….? amehoji Profesa Kinyondo.

Amesema wakati Mpina akiingia ACT – Wazalendo, tayari chama hicho kilikuwa kilikuwa na mgombea wake, ambaye ni Dorothy Semu, hivyo hatua ya kupewa kijiti nayo ilipaswa kumshitua.

“Jambo lingine, pingamizi la kwanza kwake aliwekewa na mtu wa ndani ya ACT – Wazalendo tena kiongozi mwandamizi, kwa hili pia alipaswa kushtuka, angekuwa mweledi angejua kuna mchezo hapo,” amesema Profesa Kinyondo na kuongeza: “Anayepaswa kulaumiwa kwa yanayoendelea ni Mpina mwenyewe, alipaswa kuyaona haya yanayotokea tangu mwanzo. Alipaswa kuicheza sinema anayoiona mbele yake na si kuichukulia kwa uzito mdogo.”

Naye Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Dk Richard Mbunda, amese kinachoendelea dhidi ya Mpina kinatoa taswira ya mifumo ya utoaji haki ilivyo na mapungufu.

“ACT – Wazalendo wamekuwa wakitoa ufafanuzi juu ya jambo hilo wakieleza kifungu kinachoelezwa kimeshaondolewa, tulihitaji suala kama hilo lisikilizwe na mahakama kwa sababu ndio chombo cha utoaji haki. Isivyo bahati sheria zetu zimeshaifunga Mahakama kwamba, haiwezi kuingilia maamuzi ya INEC,” amesema Dk Mbunda.

Amesema kama ni mchezo, umechezwa ni ngumu kufahamu nani mwenye haki, huenda ni kweli Mpina alikosa vigezo au kanuni zinaweza kuwa hazipo hivyo, mamlaka ambayo ingeleta majibu ya usahihi na uhalali wa Mpina, ni Mahakama.

Taarifa ya ACT- Wazalendo

Uongozi wa ACT-Wazalendo kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa leo, Septemba 15,2025 na kusainiwa na Ado Shaibu, kimesema hawakubaliani na uamuzi huo kwa kuwa haukuzingatia misingi ya sheria.

“Tume ya uchaguzi imefanya uamuzi kwa kutumia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa ambao, chama na mgombea tumeukatia rufaa katika Mahakama Kuu kupitia shauri namba 23428 la mwaka 2025 Masjala Kuu Dodoma.

“Kumuengua mgombea wetu kwa sababu zisizokuwepo kisheria ni moja ya uthibitisho wa njama na dhamira hiyo ovu dhidi yao.

“Tutaendelea kusimama imara kuhakikisha kuwa tunaihami nchi yetu dhidi ya dhamira hiyo. Kiongozi wa Chama Taifa, Dorothy Semu ameitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi ya Taifa kujadili suala hili,” imeeleza taarifa hiyo ya ACT-Wazalendo.